Zitto Kabwe Kufungua Kesi Mahakamani Kupinga Kuwa Na Mamlaka Moja tu ya Kutoa Takwimu za Taifa
Kiongozi
wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema watafungua kesi mahakamani
kupinga baadhi ya vifungu vilivyomo katika Sheria ya Takwimu ya mwaka
2015.
Akizungumza
na waandishi wa habari nje ya kitengo cha upelelezi wa makosa ya
kifedha kilichopo Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Zitto amesema
haiwezekani kukawa na mamlaka moja ya kutoa takwimu.
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini amesema tangu kutungwa kwa sheria
hiyo imekuwa ikipigiwa kelele kutokana na kuminya uhuru wa wananchi
kuchambua takwimu.
"Tunataka
kufungua kesi mahakamani kupinga sheria ya takwimu kuzuia watu
kuchambua, huko ndiko ukweli utajulikana na wananchi watajua sheria hii
ilivyo. Hii itakuwa kesi ya kwanza kwa sheria hii kupelekwa mahakamani,"
amesema Zitto.
Amesema,
"Tuna taarifa ambazo hatukuzitoa, tukifika mahakamani tutazitoa na NBS-
(Ofisi ya Taifa ya Takwimu) haiwezi kusema una hatia au la kwa kuwa wao
si Mahakama. Sisi tulitumia takwimu zao kuchambua na tumewaeleza polisi
kwamba tutawaeleza zaidi tukifika mahakamani."
Zitto
ametoa kauli hiyo siku moja baada ya jana Jumapili Novemba 5,2017
Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa kusema mtu mwenye mamlaka ya
kutoa takwimu ni ofisi hiyo pekee.
Dk
Chuwa katika kipindi maalumu kilichorushwa na kituo cha televisheni cha
Azam kuhusu miaka miwili ya utawala wa Rais John Magufuli aliyeingia
Ikulu Novemba 5,2015 alisema takwimu za Taifa ni lazima ziheshimiwe na
si kila mtu anastahili kuzitoa.
Zitto
akizungumzia tuhuma za uchochezi zinazomkabili amesema, “Nimeripoti leo
kama nilivyotakiwa lakini nimeelezwa nirudi tena Ijumaa Novemba 17,2017
wanadai wanasubiri chaji kutoka kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) na
baada ya hapo wataona kama watanipeleka mahakamani au la.''
"Lakini
kesho, mimi nitakuja hapa (kitengo cha uhalifu wa makosa ya kifedha)
saa tatu au saa nne kama nilivyotakiwa. Mtakumbuka natuhumiwa kwa kesi
mbili ya sheria ya takwimu na makosa ya mitandao," amesema.
Zitto
pia amezungumzia uamuzi wa Jeshi la Polisi la kuiita kamati kuu ya ACT-
Wazalendo akisema haina uwezo huo na wao kama walivyoeleza jana katika
mkutano na waandishi wa habari watawakilishwa na Mwenyekiti wa chama
hicho, Yeremia Maganja na Katibu Mkuu Doroth Semu.
"Polisi
hawana uwezo wa kuihoji kamati kuu, ndiyo maana mwenyekiti na katibu
mkuu wapo hapa wanaendelea na mahojiano... huwezi kuwaita wajumbe wote
wa kamati kuu kwa kuwa mtendaji wa chama ni katibu mkuu na msemaji ni
mwenyekiti na ndicho tumekifanya," amesema.
