Waziri Mkuu awataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na
utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko Serikalini.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Novemba 7, 2017) wakati akifungua Kikao
Kazi cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina
Mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu amesema ni vema viongozi hao kabla ya kutoa matamko
wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera
na kama lipo katika bajeti za wizara zao.
Pia
amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi
ili kuithibitishia jamii kuwa Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana
na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.
“Tunao
wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa
nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli
na wananchi wote kwa ujumla.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa
kusikiliza hoja na shida za Wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa
sheria, taratibu na kanuni.
Pia
amewataka wafanye ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango
mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi
wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Waziri
Mkuu amesema Mawaziri na Naibu Mawaziri wanatakiwa wasimamie
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi
2020/2021.
Pia
wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli
wakati wa kampeni za uchaguzi.
