Rais Magufuli Ameirudisha Nchi Kwa Wananchi
Na Judith Mhina – MAELEZO
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amerejesha
nchi kwa wananchi na kwamba hayo ni mapinduzi ya ajabu ambayo hayajawahi
kutokea katika nchi zetu hususan Afrika.
Maneno
hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
Dkt. Ayub Rioba alipofanya mahojiano na redio Uhuru mwishoni mwa wiki
iliyopita katika ofisi zao zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini
Dar-es-salaam.
Dkt.Rioba
amesema Mhe. Rais ameirudisha nchi kwa wananchi kwa kuwa anatekeleza
“kile anachoambiwa na wananchi, na ahadi alizowaahidi wakati akiwaomba
kura” anaeleza Dkt. Rioba na kuongeza kuwa yeye binafsi anamshukuru Mhe.
Rais kwa “kuirudishia heshima Tanzania“.
Katika
mahojiano hayo, Dkt. Rioba alieleza kuwa tangu kushika madaraka miaka
miwili sasa Rais Magufuli amekuwa ‘busy’ kuhakikisha nchi inakaa sawa
kimfumo ndio maana hajashughulika sana na safari za kwenda nje ya nchi.
Rais
anataka kutengeneza “mfumo wa kimkataba au kibiashara na hawa mabwana
wakubwa (wawekezaji toka nje) utakaowezesha kugawana nusu kwa nusu
katika kile kinachopatikana katika uendelezaji wa rasilimali zetu badala
ya mifumo ya zamani ya kukubali kila mfumo unaoletwa na nchi
zilizoendelea” alisema Dkt. Rioba.
Mkurugezi
Mkuu huyo alikieleza kituo hicho cha redio kuwa yeye binafsi anadhani
kilichosababisha Kampuni ya kuchimba Dhahabu ya Barrick kumsikiliza Mhe
Rais ni umakini wa kiongozi huyo kwa “hanunuliki, hahongwi hongwi maana
Afrika ina viongozi wengi ambao wananunuliwa na kuhongwa” lakini sasa
wanajua huyu ni tofauti.
Dkt.
Rioba anamuona Rais Magufuli kuwa kiongozi anayesimamia mambo yanayo
wanufaisha wananchi wake na “hakimbii kimbii kwenda huku na kule kuomba”
na kuifananisha nchi yetu na zile zinazotoa misaada katika nchi
nyingine. Kwa kuwa fedha wanazozipata zinatokana na rasilimali zetu na
kueendeleza nchi zao.
Mhe Magufuli alisema; “Nchi yetu ilitakiwa kuwa Donor Country, yaani nchi inayotoa misaada kwa nchi nyingine”.
Ninachoweza
kuwaambia Watanzania wenzangu miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano
madarakani, hakika viongozi wetu wameonesha nia nzuri na wanatakiwa
kuunga mkono kwa hili analolifanya Rais Magufuli wakati huu wa mpito.
Nchi
yoyote inapopita katika mpito ni lazima kuna mambo yalikuwa hayaendi
sawa na mengine yamekwenda sawa. Mpito ukitokea kuna mabadiliko
yatakayojitokeza. Mfano Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
alipendekeza mfumo wa vyama vingi japo wananchi wengi, bado waliutaka
mfumo wa chama kimoja. Aidha kutokana na kubadilishana uongozi hapa
Tanzania, mabadiliko mengi yalijitokeza ambayo yalikuwa mazuri na
mengine sio mazuri kwa kuwa ni kipindi cha mpito.
Dkt.
Rioba amesema ujio wa Rais Magufuli ulikuwa ujio muhimu sana kwa wakati
huu, kwa ajili ya kurekebisha yale yote yaliyojitokeza ambayo hayakuwa
sawa. Akitoa mfano wa mwana falsafa mmoja anayeitwa Fans Fanon wakati wa
vita vya ukombozi nchini Algeria alisema:
“Kila kizazi kinakutana na majukumu yake ya msingi ya kutekeleza au kuyatelekeza na kusubiri matokeo yake”
Mkurugezi
Mkuu huyo wa TBC alieleza kuwa kwa maoni yake Rais Magufuli amekuwa
kiongozi sahihi aliyekuja kwa wakati sahihi, ili kurekebisha mambo kwa
namna moja au nyingine ambapo hapa na pale tulijikwaa kwa sababu
tulitoka nje ya misingi iliyojengwa na Taifa letu.
Kuhusu
suala la kuwa na uchumi mzuri katika nchi Rioba amesema tafiti
zinafanyika kwa mrengo wa kimagharibi zaidi ambapo, wanahalalisha mifumo
ya uchumi wanayoitaka wao. Wachumi walio wengi wanasema ili uchumi uwe
mzuri na nchi kuendelea ni lazima kuwa na Ardhi, tekinolojia, rasilimali
ziwe nyingi nk , lakini sio kweli.
Mfano
nchi ya Singapore hawana rasilimali zaidi ya bahari na samaki lakini
uchumi wao ni mzuri sababu moja kubwa ni uongozi bora ambao unasimamia
matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya wananchi wa nchi husika.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya 4 duniani kwa wingi wa
madini lakini haijaendelea, mpaka leo kuna watu wanaomiliki madini
katika nchi hiyo wako nje hivyo faida yote inayopatikana kutokana na
madini hayo inazinufaisha nchi za nje.
Jambo
la msingi Rais Magufuli anataka rasilimali zilizopo, hata kama kidogo
kitumike kwa manufaa ya wananchi wanyonge wa Tanzania. Tanzania ya Rais
Magufuli amesema hapana haya madini yanayopatikana hapa Tanzania ni
lazima tugawane nusu kwa nusu.
Dkt.
Rioba anasema Rais ameonesha mfano kwa nchi nyingine za Afrika zenye
rasilimali kama zetu, kuwa hili la kugawana faida nusu kwa nusu, hata
kama hatuna tekinolojia na mitaji linawezekana.
Zipo
nchi nyingi za Afrika ambazo zilitumia rasilimali zao vibaya mfano,
Siera Leoni, Liberia wakawa wanachimba almasi kwa ajili ya kuendesha
vita na kununua silaha kutoka nchi zilizoendelea. Afrika ifike mahali
ioneshe ukomavu na kuacha mambo ya kipumbavu kama hayo ioneshe kuwa
Afrika ina watu wanaweza kufikiri na kuweza kugawana rasilimali kama
alivyofanya Rais Magufuli.
Ukiangalia
nchi ya Nigeria asilimia 80 ya mafuta yanayosafirishwa kwenda nje ni
asilimia 1 tu ya mafuta hayo ndio yanarudi Nigeria, lakini Tanzana ya
Magufuli amesema hapana
Akitoa
mfano Dkt Rioba alisema Baba wa Taifa mara baada ya Uhuru wa
Tanganyika, wasomi walikuwa wachache sana wasingeweza kutosheleza katika
masuala ya utaalam na kuleta maendeleo kupitia rasilimali tulizonazo.
leo hii nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika suala la taaluma na
elimu ambapo hatukuwa na Chuo Kikuu hata kimoja. Leo Tanzania ina vyuo
vikuu takriban 50, na wataalamu wako wengi, tunachokosa ni Wataalamu
wanaoipenda nchi yao wazalendo wenye nia ya kusukuma gurudumu la
maendeleo.
Dkt.
Rioba anaeleza kuwa ni vizuri kuwa na waaalam vijana wenye moyo wa
kujituma na uzalendo na kuwa tayari kuwa watumishi wa wananchi na
kusaidia kutimiza ndoto ya Tanzania ya viwanda na ndivyo anavyotaka
Rais Magufuli.
Akizungumzia
suala la kuondoa dhana ya kuwa na matabaka ya watu katika Taifa, Rioba
amesema kwa sababu Tanzania iko katika mpito, ambapo ilitoka katika
misingi ya Ujamaa na Kujitegemea (Azimio la Arusha) na sasa ni kama
kutengeneza Azimio la Arusha jipya lakini katika muktadha wa zama za
sasa. Kwa wale watanzania ambao ni wazalendo kabisa kabisa, Dkt. Rioba
anasema watakubaliana nae kuwa anayoyafanya Rais Magufuli ni lazima
aungwe mkono kwa kuwa anaipeleka nchi panapostahili.
Dkt.
Rioba katika mahojiano hayo amesema ni wakati sasa kwa kila Mtanzania
kuona uchungu kwa kila aina ya wizi wa rasilimali za nchi na kwamba
dhambi kubwa ambayo watanzania wanaweza kuifanya ni kudhani kuwa jukumu
la kulinda rasilimali za nchi ni la Rais Magufuli pekee.
“Haijawahi
tokea kiongozi yeyote barani Afirika kusema wananchi tumeibiwa mno na
mbali zaidi, kutafuta suluhisho la kuibiwa huko. Hongera Rais Magufuli
jitihada zako ni ukombozi kwa rasilimali zote Barani Afrika na mwisho wa
Bara la Afrika kuwa Shamba la Bibi (akimaanisha kila mtu anakuja
kujichukulia na kundoka)” Dkt. Rioba alimazilia mahojiano hayo.
