RAIS MAGUFULI AANZA ZIARA YA SIKU NNE MKOA WA KAGERA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
leo tarehe 06 Novemba, 2017 ameanza ziara ya kikazi ya siku 4 katika
Mkoa wa Kagera.
Akiwa njiani Kutoka Chato Mkoani Geita alikokuwa mapumzikoni kuelekea
Bukoba Mjini Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Muleba na
Kemondo, Bukoba Vijijini na kuwahakikishia kuwa Serikali itasaini
mkataba na kampuni ya kutoka Jamhuri ya Korea kati ya mwezi Desemba
mwaka huu na Januari mwakani kwa ajili ya kuanza kuunda meli mpya katika
ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya abiria na
mzigo mkubwa zaidi ikilinganishwa na meli zilizopo
“Tunaunda meli ya kisasa itakayobeba abiria wengi na mizigo mingi, na
pia tutakarabati meli zilizopo za MV Victoria na MV Butiama, tunataka
pamoja na kujenga barabara, tuhakikishe kuna meli za uhakika ili muweze
kusafiri na kusafirisha mazao yenu kwenda kwenye masoko” amesema Rais
Magufuli.
Kuhusu ufugaji Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera
kuhakikisha mifugo yote inawekwa alama kwa mujibu wa sheria, ili
kurahisisha utambuzi wa mifugo inayoingizwa nchini kutoka nchi jirani na
pia kudhibiti ruzuku inayotolewa na Serikali kwa dawa za mifugo ya hapa
nchini.
“Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani, ndio maana
tumeamua kukamata mifugo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kisheria, na
hata huko kwenye nchi jirani wakishika mifugo ya kutoka Tanzania
wachukue hatua za kisheria za nchi hizo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo amewataka wananchi wa Kagera kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi
ikiwemo hifadhi ya Burigi na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Muleba
kufuatilia madai ya wananchi juu ya kuuzwa kwa ardhi ya kijiji
kulikosababisha wananchi kukosa maeneo ya kulima na kulisha mifugo yao.
“Na kuna watu waliouziwa ranchi na Serikali, watu hao hawajaziendeleza
ranchi hizo na badala yake wanawakodisha wananchi, wafuatilieni na
mkiona hawajaziendeleza nyang’anyeni muwape wananchi wazitumie kwa
ufugaji, lakini pia hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi
yaliyotengwa” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa na Wilaya za Mkoa
wa Kagera kuwachukulia hatua maafisa wote wa halmashauri ambao bado
wanawatoza ushuru wakulima wanaosafirisha mazao yaliyo chini ya tani
moja kwa kuwa tayari Serikali imeshaamua kuondoa adha hiyo na
kuwawezesha wakulima wadogo kunufaika na kilimo chao.
Mchana wa leo (06 Novemba, 2017) Mhe. Rais Magufuli atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Bukoba
06 Novemba, 2017
