Waziri Mkuu: Watakaokwamisha Malipo Ya Korosho Kukiona
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote watakaokwamisha malipo ya wakulima wa zao la korosho.
“Hatutamuacha
mtu yeyote atakayesababisha wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao.
Tutawakamata wote na kuwachukulia hatua stahiki.”
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) alipozungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mbekenyera wilaya
ya Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri Mkuu alisema wakulima hao ni lazima walipwe fedha zao kwa wakati na asitokee mtu wa kuzitamani fedha hizo.
“Mkulima
amelima mikorosho mwenyewe, ameokotoa na kukodoa mwenyewe wao wamepewa
dhamana ya kuziuza, hivyo wahakikishe wanawapelekea fedha zao na wala
wasizitamani.”
Pia
Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya Ushirika vya Msingi
wahakikishe mkulima hakosi sh. 3,500 katika kilo moja ya korosho
atakayoiuza baada ya kukatwa michango.
Alisema
bei ya juu ya korosho katika minada ya mkoa wa Lindi sh. ni 3,970 na ya
chini sh. 3,800. “Vyovyote itakavyokuwa mkulima hawezi kukosa sh.
3,500, viongozi wa AMCOS mnisikie.”
Waziri
Mkuu alisema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa bei ya zao la
korosho pamoja na kupungua kwa makato ya mkulima ambapo kwa sasa
hayazidi sh. 300 katika kilo moja ya korosho.
