RAIS MAGUFULI ATAJA SABABU ZA KUCHELEWA KUTEUA JAJI MKUU TANZANIA
Rais John Magufuli amefichua siri ya kumteua Profesa Ibrahim Juma kuwa
Kaimu Jaji Mkuu akisema hakuwa na historia ya kutosha ya majaji wengi
alipoingia madarakani.
Amesema alipoingia madarakani ilikuwa kipindi kifupi ambacho aliyekuwa
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alistaafu hivyo ilimlazimu achukue muda
mrefu wa kujiridhisha na alitumia Ibara ya 118 (4) kumteua Kaimu Jaji
Mkuu.
Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatatu, Ikulu jijini Dar es Salaam
wakati wa kumwapisha Jaji Mkuu, Profesa Juma baada ya kumteua jana
Jumapili.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Nilifanya hivi si kwa sababu hakuna majaji au walikuwa hawafai, majaji
wote ni wazuri na mnafanya kazi nzuri sana lakini sikutaka kuteua jaji
baada ya mwaka mmoja nateua tena au baada ya miaka miwili anastaafu,
nilitaka nikiteua akae miaka hata 10, awe ‘anatujaji’ wote
tutakaokuwepo,” amesema Rais Magufuli.
Amesema kumteua Jaji Mkuu ni kazi ngumu, lazima ujue historia na tabia
zake, pia kuangalia iwapo ataweza kuendana na dhamira yake ya kupambana
na rushwa.
Rais Magufuli amesema rushwa ipo kila sehemu, hivyo baada ya kuchaguliwa
na wananchi mwaka 2015 alikaa chini na kumwomba Mungu apate kiongozi
atakayeenda kulisimamia jambo hilo kwa kipindi kirefu zaidi.
Amesema wapo majaji wengi na wenye sifa lakini baadhi yao wamebakisha muda mchache kustaafu.
“Katika kufanya uchambuzi wangu nikamwona Profesa Juma ambaye alikidhi
vigezo vyangu. Nakupongeza sana Profesa Juma ni Mungu ambaye amekuchagua
kwa hiyo, kawatumikie vizuri watu wa Mungu na utangulize mbele masilahi
ya Watanzania,” amesema.
Rais Magufuli amesema ingawa bado kuna changamoto mbalimbali katika
Mhimili huo, alimuhakikishia Profesa Juma kwamba Serikali inazitambua na
aliwataka majaji kutembea kifua mbele kwa kuwa Serikali inatambua kazi
nzuri wanayoifanya.
Amesema kazi nzuri yoyote haikosi watu wa kuiponda, akitumia msemo wa mti wenye matunda ndiyo unaopopolewa kwa mawe.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema alipomteua kuwa Kaimu Jaji alipondwa
lakini alikuwa mvumilivu na hakupata shinikizo la mtu yeyote la kumteua
Jaji Mkuu.
