BUNGE LAAHIDI KUMPA USHIRIKIANO JAJI MKUU TANZANIA
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefunguka na kudai atahakikisha
yeye na wabunge wanampa ushirikiano Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma
aliyeapishwa leo baada ya kuteuliwa siku ya jana Septemba 10 mwaka huu.
Ndugai ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anatoa salamu za wabunge
katika ghafla hiyo ya uapisho iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu
Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa
bila ya kumsahau Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
"Sisi kama bunge tunawahakikishia ushirikiano mkubwa sana kwa
kuhakikisha kazi za Mahakama zinaendelea kama zilivyo kikatiba na
tutaheshimu sana. Yale maneno na makombora moja moja ya bungeni ni vitu
vya kawaida, ndiyo utamaduni wa bunge",amesema Ndugai.
Aidha, Ndugai amesema Mahakama inamchango mkubwa kwa wananchi pamoja na
taifa kwa ujumla kwa kuwa hicho ndicho chombo pekee kinachoweza kumtetea
mnyonge kuweza kupata haki yake kutoka kwa waporaji.
"Kuwepo kwa Mahakama ndiyo usalama wetu, amani, kheri na matumaini ya
mnyonge katika sheria na maamuzi ya Mahakama. Kwa hiyo tunakutakia kila
la kheri katika kazi yako, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu na
tutakusaidia na kuomba msaada wako",amesisitiza Ndugai.
Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma ameahidi kufanya
kazi katika maadili ya kisheria pamoja na kurudisha imani ya wananchi
kuhusiana na kupata misaada ya kisheria inayotolewa katika Mahakama
mbalimbali ndani ya Tanzania
