HALMASHAURI YA KISHAPU YATENGA BAJETI YA MILIONI 4.7 KUSAIDIA TAULO LAINI 'PEDS' KWA WANAFUNZI WALIOKO KWENYE HEDHI
Halmashauri
ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imetenga bajeti ya shilingi
milioni 4.7 katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kununua taulo
laini ‘Peds’ kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule zote za
sekondari wilayani humo kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi.
Akizungumza
leo Alhamis Septemba 7,2017 kwenye Tamasha la Jinsia la 14 mwaka 2017
lililoandaliwa na TGNP Mtandao linalofanyika jijini Dar es salaam,Afisa
Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya Kishapu,Joseph Swalala alisema
hatua hiyo itawasaidia wanafunzi wengi kuhudhuria masomo yao shuleni.
Swasala
alisema wanafunzi wengi wa kike wanapokuwa katika hedhi hushindwa
kuhudhuria masomo yao shuleni kwa wastani wa siku tatu kwa mwezi kwa
vile huchukulia kuwa hedhi ni ugonjwa.
“Madiwani
katika halmashauri yetu wamekubali kupitisha bajeti ya shilingi milioni
4.7 kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya taulo laini kwa
wanafunzi wa kike katika shule za sekondari,na tutaanza na wanafunzi
256”,alieleza Swalala.
“Tulibaini
kuwa hedhi ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto wa kike
kutohudhuria masomo yao hivyo kushindwa kufaulu vizuri kwenye mitihani
yao”,aliongeza Swalala.
Alisema
wanachofanya hivi sasa ni kuhakikisha katika kila shule kunawepo na
vyumba maalumu kwa ajili ya watoto kujistiri lakini kuwa na walimu
walezi kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi.
Akizindua
Tamasha la Jinsia mwaka 2017,Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan alikabidhi tuzo kwa Halmashauri ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na
Kisarawe mkoa wa Pwani kwa kutenga bajeti inayozingatia masuala ya
Kijinsia hususani suala la Hedhi Salama kwa watoto wa kike shuleni.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
