FAMILIA YASUSA MAZISHI YA MTEKAJI WA WATOTO
Familia ya marehemu Samson Petro imefunguka na kusema haitofanya matanga
wala kuufuata mwili wa marehemu kutokana na kitendo cha ukatili
alichokifanya na kusema kuwa ni kitendo kisichoweza kuvumilika na
wanaamini kuwa mwili huo haustaili kuzikwa.
Hayo yalizungumzwa na Petro Aaron, ambaye ni baba mzazi wa marehemu
Samson mbele ya wanafamilia wengine akiwepo mama mzazi wa marehemu huyo,
amesema kitendo kilichofanywa na marehemu si kitendo cha kusameheka
wala kusahaulika katika jamii.
Marehemu Samson anatuhumiwa kwa kosa la utekaji na mauaji ya watoto
wawili ambaye ni Moureen Njau na Ikhram Salim ambapo aliwaua na
kuwatumbukiza katika mtaro wa maji machafu.
Aidha kamanda wa polisi mkoani Arusha , Charles Mkumbo ameeleza kuwa
mtuhumiwa huyo alikamatwa siku ya jumatano iliyopita na kutaka kutoroka
ndipo polisi walipoamua kumjeruhi miguu yote miwili.
Kutokana na majeraha hayo, mtuhumiwa alipoteza damu nyingi na kumpelekea mauti kumkuta.
‘’ Mtuhumiwa alijaribu kutoroka, ndipo polisi walipolazimika kumjeruhi
miguu yote miwili na kukimbizwa hopsitali ya Mkoa Mount Meru
akibubujikwa na damu ndipo alipofariki dunia.
Tukio hilo lilitokea baada ya mtuhumiwa Samson, kukubali kuonesha eneo
alilokuwa akiishi kijana mwingine aliyeshirikiana naye katika kufanya
uhalifu huo.
