Waziri Mkuu: Hospitali Zote Za Mikoa Zijenge Vituo Vya Methadone
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amegiza hospitali zote za mikoa nchini kujenga
vituo vya kutolea huduma ya Methadone kwa ajili ya kuwahudumia
waathirika wa dawa za kulevya.
Alitoa
agizo hilo Jumatatu, Julai 31, 2017 alipozindua kituo cha kuhudumia
waathirika wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambapo
alisema Serikali inaendelea na mpango wake wa kudhibiti uingizwaji wa
dawa hizo.
Kituo
hicho kinatarajiwa kuhudumia watumiaji wa dawa za kulevya katika mikoa
yote ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi,
Rukwa, Songwe na Mbeya.
Waziri
Mkuu alisema vituo vya kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya ni
msaada mkubwa kwa vijana kwa kuwa mbali na kupewa dawa pia watafundishwa
stadi za maisha ili wanapomaliza matibabu waweze kushiri katika
shughuli za maendeleo ikiwemo kujiajiri.
Hata
hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuwafichua wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya
kwa sababu ni watu wanaoishi nao katika jamii.
Kwa
upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za
Kulevya, Rodgers Sianga alisema licha ya matumizi ya dawa za kulevya
kuathiri mfumo wa fahamu pia watumiaji wako katika hatari ya kuugua homa
ya ini.
Alisema
vituo hivyo licha ya kutoa dawa ya methadone pia waathirika wa dawa za
kulevya ambao watagundulika kuwa na maradhi mengine kama ukimwi, kifua
kikuu, matatizo ya kisaikolojia pamoja na homa ya ini pia watatibiwa
katika vituo hivyo.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dkt.Godlove Mbwanji alisema
matumizi ya dawa za kulevya yamechangia ongezeko la wagonjwa wa akili
mkoani Mbeya, ambapo mwaka jana pekee walibainika wagonjwa 486.