Mkemia: Mkojo wa Wema Sepetu Ulikuwa na Bangi
Kesi
ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi inayomkabili mrembo Wema
Sepetu jana aliendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu ambapo shahidi namba moja kwa upande wa mashtaka alitoa ushahidi
wake na kusema kuwa mkojo wa mrembo huyo ulionyesha kuwa alivuta bangi.
Shahidi
huyo, Elias Mulima kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akiongozwa
na wakili wa serikali Constantine Kakula aliieleza mahakama hiyo mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba namna alivyompima mtuhumiwa huyo na
kubaini kuwa mkojo wake ulikuwa na bangi ambapo sampuli ya mkojo huo
aliipokea Februari 8.
Shahidi
alisema baada ya Wema kutoa sampuli ya mkojo huo ilipelekwa maabara
ambapo lengo lilikuwa ni kuchunguza chembechembe za uwepo wa dawa za
kulevya na ndipo walipobaini uwepo wa dawa za kulevya aina ya bangi.
Baada ya kutoa ushahidi huo, Elias alitoa taarifa ya uchunguzi
aliyoiandaa na kuisaini yeye mwenyewe na pia kuthibitishwa na kaimu
mkemia mkuu wa serikali ili itumike kama kielelezo cha ushahidi.
Baada
ya hoja hizo, upande wa utetezi unaoongozwa na Wakili Peter Kibatala
aliitaka mahakama kutopokea taarifa hiyo kwa sababu uchunguzi haukufuata
sheria kwani Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai inataka uchunguzi
wa kitabibu kwa mtuhumiwa ambaye yupo chini ya ulinzi lazima upate
kibali cha mahakama.
Aidha alitaka pia mahakama isipokee taarifa hiyo kwa sababu haikumbatanaishwa na fomu namba DCEA 001.
Akijibu
hoja hizo, hakimu aliyekuwa mahakamani hapo alisema kuwa, fomu yenye
namba 001 inatumiwa na Polisi wanaopeleka sampuli na fomu namba 009 ni
taarifa ya mkemia, na kwamba fomu moja haitegemei nyingine kwa sababu
huandaliwa na watu tofauti.
Hakimu
pia aliipangua hoja ya Kibatala ya kibali cha mahakama ambapo alisema
sheria haijasema kuwa wakati wote lazima Polisi waombe kibali hicho cha
uchunguzi wa kitabibu, lakini pale ambapo mtuhumiwa atakuwa hayupo
tayari, wanaweza kuomba kibali cha mahakama.
Kutokana
na mvutano ulioibuka mahakamani hapo kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi,
mahakama iliomba muda wa kupitia nyaraka hizo na kesi hiyo ikaahirishwa
hadi Agosti 4 mwaka huu.