Taasisi za umma zabanwa kuhusu matumizi ya kuni na Mkaa.......Hapa Kuna Tamko Lililotolewa na Waziri Makamba

Kama mnavyofahamu zaidi ya asilimia 90 ya watanzania nchini wanatumia mkaa na kuni kama nishati ya kupikia na mwanga. Pamoja na kuwapo kwa vyanzo vingine mbadala vya nishati nchini, bado mahitaji ya ni shati ya mkaa na kuni yataendelea kuongezeka kadiri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka nchini. 

Hali hi iinasababisha changamoto kubwa katika suala zima la hifadhi ya misitu ya asili na mazingira kwa ujumla. Mahitaji ya nishati ya mkaa ni makubwa katika meaneo ya mijini na yataendelea kuongezeka. 

Ni kwa muktadha huu, mnamo mwezi Novemba, 2016 Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa warsha ya wadau kwalengo la kujadiliana, kushauriana na kutoa mapendekezo ya njia na mbinu endelevu za kupunguza matumizi ya mkaa hasa utokanao na miti ili kuokoa misitu yetu na mazingira kwa ujumla. 

Aidha warsha hii pia iliyojumuisha viongozi wa Wizara za Maliasili naUtalii,na Nishati na Madini; Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine; taasisi zisizo za serikali zinazojishughulisha na mkaa mbadala; kampuni zinazofanyabiashara ya gesi ya mitungi; n.k. Vile vile warsha hiyo ilikua na lengo la kuangalia njia bora za kuhamasisha uzalishaji wa mkaa kwa njia endelevu pamoja na kuzalisha mkaa kwa njia mbadala za kutumia masalia mbalimbali badala ya kutumia miti.

Ndugu Wananchi;
Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira Nchini ambayo ilichapishwa mwaka 2014 imebaini kuwa licha ya Serikali na wadau wengine kuwa na mipango mingi na mizuri, hali ya mazingira si ya kuridhisha. 

Vilevile kutokana na Taarifa ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali za Misitu Nchini (National Forest Resources Monitoring and Assessment (NAFORMA)) ambayo inaonyesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu nchini ni kubwa sana ambapo kiasi cha hekta 372,000 (au ekari takribani milioni moja) za misitu zinaangamizwa kila mwaka.Uhariblifu huu unasababishwa kwa kiwango kikubwa na mahitaji ya nishati hasa ya mkaa na kuni. 

Mahitaji ya mkaa nchini ni ya juu mno na yataendelea kuongezeka kadri idadi ya watu inavyoendelea kuongezeka hapa nchini. Kwa mfano, katika Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira (2014), Jiji la Dar es Salaam linatumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka na mahitaji haya yanaweza kuongezeka kadri jiji linavyoendelea kupanuka.

Taasisi za Serikali Kutumia Gesi Kupikia

Ndugu Wananchi;

Ni dhahiri kwamba Serikali ni moja ya mtumiaji mkubwa wa kuni na mkaa katika taasisi za umma zenye kukusanya watu wengi (mashule, vyuo, magereza, kambi za jeshi, nk). 

Katika kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni, Serikali lazima Katika kukabiliana na changamoto ya matumizi ya mkaa nchini,  nimefanya vikao kadhaa wa wadau mbalimbali, ikiwemo jumuiya ya wazalishaji na wasambazaji wa gesi ya kwenye mitungi (liquefied petroleum gas -LPG). 

Katika mazungumzo yetu tumefanikiwa kuwashawishi makampuni ya kuuza na kusambaza gesi ya kupikia nchini kufunga mitambo ya kuhifadhi gesi na majiko ya gesi katika taasisi za Serikali ambazo ni watumiaji wakubwa wa nishati ya mkaa na kuni ili kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira. 

Aidha, makampuni haya yamekubali kufanya hivyo bila gharama yoyote ile ya ufungaji wa mitambo hiyo. Taasisi zitakazohusika na kunufaika na mpango huu ni pamoja na shule, vyuo, magereza, makambi ya jeshi na hospitali. 

Aidha, ili kufanikisha suala hili, tumefanya uchambuzi wa bei na gharama za kufunga mitambo hiyo na uchambuzi huo umeonesha kwamba hatua hii itapunguza gharama kwa taasisi husika na pia itachangia kupunguza mahitaji ya ukataji miti kwa ajili ya kuni au/na mkaa na hivyo, kuchangia katika kuhifadhi mazingira. Kwahivyo basi, tumeziandikia barua taasisi hizi ziwaelekeze wazabuni wake wa kupika kuhusu mahitaji ya kubadilisha nishati ya kupikia. Barua zetu zinatoa utaratibu mahsusi wa utekelezaji wa suala hili. 

Maelekezo haya tumeyatoa kwa mamlaka tuliyopewa na Sheria ya Mazingira ya 2004, kifungu cha 13. Matumaini yetu ni kwamba ndani ya mwaka mmoja taasisi zote za umma zitakuwa hazitumii kuni wala mkaa. Vilevile, kwa taasisi ambazo zinaweza kuunganishwa na mfumo wa gesi ya CNG pale ambapo mfumo utakuwa umejengwa. 

Mwongozo (Road Map) ya Kuondokana na Matumizi ya Mkaa

Ndugu Wananchi;

Kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya mkaa nchini na athari yake katika mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya warsha ya mkaa iliyofanyika mwaka jana,imechukua jukumu la kuratibu maandalizi ya mpango wa kuondokana na matumizi ya mkaa hapa nchini. 

Ili kufanikisha mpango huo, wadau mbalimbali wakiwemo Sekta binafsi, Taasisi zisizo za Kiserikali, Wizaraza Serikali, Serikali zamitaa, Taasisi za Serikali, Sekta binafsi, Makampuni ya mafuta na Gesi, makampuni yanayotengeneza mkaa mbadala na wanaojihusisha na juhudi/teknolojia ya kupunguza matumizi ya mkaa utokanao na misitu yetu watashirikishwa. 

Mpango huo utatoa dira, mwelekeo na ratiba yakuondokana mkaa nchini nawajibu wa wadau wote. Pia utaelekeza kuhusu fursa za uchumi, ajira nakipato zilizopo katika uchumi wa mbadala wa mkaa. Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Mazingira kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais wataratibu Mpango huu.

Aidha, mwishoni mwa mwaka 2017 Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuandaa na kuratibu maonesho makubwa ya juhudi pamoja na teknolojia za kupunguza matumizi ya mkaa zinazotekelezwa na wadau mbalimbali hapa nchini.

Maonyesho haya yatakuwa ni sehemu ya mashindano ya kubuni mbadala wa nishati ya mkaa wa kukatamiti. Maelezo zaidi yatatolewa katika wiki chache zijazo.

JANUARY Y. MAKAMBA (MB)
WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA
Powered by Blogger.