Serikali Yazidi Kujibu Mapigo ya CHADEMA......Yasisitiza Uchumi wa Tanzania ni Imara na Tunaongoza Afrika Mashariki
By Bushiri Matenda-MAELEZO
Licha
ya kuyumba kwa uchumi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani,
Tanzania imeendelea kuongoza kwa ukuaji wa uchumi miongoni mwa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo takwimu za Benki Kuu ya Tanzania
(BOT) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimetaja uchumi wa Tanzania
kuwa imara.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan
Abbasi alibainisha hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari
jana Jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya uchumi nchini.
“Uchumi
wa Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo sasa bado uko katika ukuaji
usiopungua asilimia 7.0 hadi 7.2 ikiwa ni ukuaji wa juu katika ukanda wa
Afrika Mashariki ambapo Rwanda inakua kwa asilimia 6, Uganda asilimia 5
na Kenya asilimia 6.4”, alisema Dkt. Abbasi.
Alieleza
kuwa sambamba na ukuaji wa uchumi, Tanzania imeendelea kudhibiti
mfumuko wa bei ambapo taarifa ya hivi karibuni zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kuwa mfumuko wa bei nchini umeshuka
kutoka asilimia 6.1 mwezi Mei hadi kufikia asilimia 5.4 mwezi Juni mwaka
huu.
Aidha,
Mkurugenzi Dkt. Abbasi alieleza kuwa katika eneo la mazingira bora ya
uwekezaji, Tanzania imeendelea kufanya vizuri ambapo alitoa takwimu za
taasisi ya Quantum Global Research Lab ya Uingereza kuhusu Farihisi ya
Uwekezaji Afrika ambazo zilionesha Tanzania ikiongoza miongoni mwa nchi
za Afrika Mashariki na ya nane Barani Afrika, ikiwa imepanda kutoka
nafasi ya 19 mwaka 2015.
“Mashirika
ya Kimataifa kama IMF, Benki ya Dunia katika ripoti zao za hivi
karibuni yamesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania ni imara na wamesifu
mageuzi makubwa yanayofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli”, alieleza
Dkt. Abbasi na kusema kuwa mashirika hayo yameitaka Serikali iendeleze
mapambano zaidi dhidi rushwa na udhibiti wa mapato ya Serikali.
Alieleza
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanyia kazi maoni hayo ya
IMF na Benki ya Dunia na kwamba mabadiliko makubwa yamefanyika katika
kupambana na rushwa na kudhibiti mapato ya Serikali ambapo ukusanyaji wa
mapato umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 925 kwa mwaka
2015 hadi shilingi trilioni 1.069 kwa mwaka 2016/17 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 15.
Dkt.
Abassi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alieleza kuwa kutokana
na uchumi wa Tanzania kuwa imara kumeiwezesha Serikali kufanya maboresho
makubwa katika sekta mbalimali zikiwemo afya, elimu, miundombinu na
nishati ambapo katika sekta ya afya Serikali imetenga shilingi trilioni
1.077 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kulinganisha na shilingi bilioni 796
zilizotengwa mwaka fedha 2016/17.
Alieleza
kwa kwa upande dawa na vifaa tiba, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea
kutekeleza ahadi yake kwa kuongeza fedha katika ununuzi wa dawa ambapo
katika kipindi cha miaka mitatu fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba
zimeongezea kutoaka shilingi bilioni 30 mwaka 2015/16 mpaka kufikia
shilingi bilioni 261 katika bajeti ya mwaka 2017/18.
“Katika
kuhakikisha Watanzania wengi wanaelimika, Serikali imeendelea kutoa
elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne ambapo takribani
shilingi bilioni 18 hutumika kwa mwezi na zinawafikia walengwa na kwa
wakati”, alieleza Dkt. Abbasi na kuongeza kuwa wakati Serikali ya
Awamu ya Tano inaingia madarakani kulikuwa na shilingi bilioni 341 kwa
ajili ya mikopo ya elimu ya juu lakini Rais John Pombe Magufuli
akaongeza hadi kufikia shilingi bilioni 475 na kwa mwaka 2016/17 bajeti
ya mikopo ya elimu juu iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 483.
Alieleza
kuwa kutokana na uchumi imara, Tanzania imeendelea kutekeleza miradi
mbalimbali mikubwa ya maendeleo ikiwemo ile ya umeme, maji, reli ya
kisasa, barabara na pia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima
nchini Uganda mapka Tanga nchini Tanzania, ambapo mradi huu unatekelezwa
kwa pamoja na nchi hizo mbili.