Afariki Kanisani Baada ya Kutoa Sadaka
Mkazi
wa Mtaa wa Makanyagio katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Beatrice
Kangu (48) amekufa muda mfupi baada ya kutoa sadaka katika ibada ya
Jumapili iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda
kilichopo katika Mtaa wa Makanyagio B.
Akizungumzia
mkasa huo, Mwenyekiti wa kigango hicho, Charles Kanyanda alisema Kangu
ambaye ni mwanakwaya, alikuwa muumini wa Kanisa Katoliki, na Jumapili
alihudhuria ibada ya Misa Takatifu kwenye kigango hicho ambayo
ilifanyika saa moja na nusu asubuhi.
Alisema
Beatrice alihudhuria ibada ya misa hiyo ambapo kwa kuwa alikuwa
mwanakwaya aliingia kwenye nyumba ya ibada na kujiunga na wanakwaya
wenzake iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu wa Dini (Katekista) wa Kigango,
Agustino Ntalwila.
“Ibada
ya Misa Takatifu iliendelea kama kawaida na ndipo ilipofikia muda wa
kutoa sadaka na Beatrice alikwenda kutoa sadaka kama kawaida kisha
akarudi kwenye nafasi yake na kuendelea kuimba ghafla baadaye alianguka
na kupoteza fahamu.
Taharuki iliibuka kwenye nyumba hiyo ya ibada ndipo ilipobainika kuwa alikuwa amekata roho,” alieleza Kanyanda na kuongeza kuwa wanakwaya wenzake walijitahidi kumpatia huduma ya kwanza bila ya mafanikio.
Kanyanda
alisema maziko yake yalifanyika katika makaburi ya Mwanga jana ambayo
yaliongozwa na Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Maria Imakulata,
Monsinyori, Padri George Kisapa aliyemwelezea alikuwa mcha Mungu na
ameacha pigo kubwa kwenye kwaya ya Kigango cha Makanyagio B.