Rais Magufuli ameiagiza JKT kurejesha ardhi kwa wanakijiji baada ya kushindwa kuiendeleza
Rais
John Magufuli ameagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kurejesha eneo la
eka 50 walilopewa na Kijiji cha Mkata, baada ya kushindwa kuliendeleza
kwa miaka saba.
Rais
ameagiza hatua hiyo ichukuliwe leo Alhamisi, Agosti 3 wakati alipokuwa
akizungumza na wananchi wa Mkata akiwa njiani kuelekea mkoani Tanga,
ambapo alimwita Mkuu wa JKT wa eneo hilo na kumhoji kuhusu kuendeleza
eneo hilo.
“Hili
eneo tangu mmepewa ni miaka mingapi sasa? Mliomba ili mjenge muwekeze
kwa kujenga kiwanda, lakini mmeshindwa sasa leo hii mrejeshe kwa
wananchi ili waweze kumpa hata mwekezaji mwingine,” ameagiza Rais Magufuli na kushangiliwa na wananchi.
Amemweleza
mkuu huyo wa JKT kwamba wakajenge kiwanda hicho kwenye kambi yao kwa
kuwa wana eneo kubwa ambalo linatosha pia kwa uwekezaji huo.
Awali
aliwataka wananchi hao kuwa na subira kuhusu ujenzi wa hospitali katika
eneo hilo, kwa kuwa kuna shaka kwamba Sh500 milioni zilizotolewa kwa
awamu ya kwanza zilitafunwa, hivyo kabla ya kuleta nyingine wanapaswa
kujiridhisha na matumizi yaliyofanywa.
Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu alipopewa nafasi ya kulitolea ufafanuzi jambo
hilo amesema wanaunda kamati ambayo itachunguza matumizi ya fedha hizo
ndipo waweze kuruhusu fedha zingine zipelekwe ili kuendeleza mradi huo.
Rais
Magufuli yupo safarini ambapo Agosti 5 atakutana na Rais Yoweri Kaguta
Museveni kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa bomba la
kusafirisha mafuta Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.