Mbunge CHADEMA Aendelea Kusota Rumande......Alikamatwa Jana kwa Tuhuma za Uchochezi
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema bado wanaendelea
kumshikilia Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga na watamfikisha mahakamani
baada ya kukamilisha upelelezi.
Kamanda
Nyange amesema sababu za kumtia mbaroni Haonga ni kutokana na kufanya
mkutano bila kibali cha polisi katika mji mdogo wa Mlowo-Mbozi na
kuwahamasisha wamiliki wa malori na abiria kuandamana kwenda ofisi ya
Mkuu wa Mkoa huo, Chiku Galawa.
Amesema
Haonga alifanya mkutano huo jana Jumatano, Agosti 2 na alihamasisha
madereva wa malori, wamiliki na abiria waende kumuona mkuu wa mkoa.
Amesema
lengo la mbunge huyo kuwataka watu hao wamuone mkuu wa mkoa ni kueleza
kero yao juu ya adha ya usafiri baada polisi kupitia kitengo cha
usalama barabarani kupiga marufuku malori kubeba abiria kutoka katikati
ya mji wa Mlowo kwenda maeneo tofauti ya vijijini ambako hakuna usafiri
mbadala zaidi ya malori.
“Bado
hatujakamilisha upelelezi na tutakapokamilisha muda wowote tutamfikisha
mahakamani na kuhusu dhamana tutafikiria kumpatia dhamana ama laa,” amesema Kamanda Nyange.