Watanzania Watakiwa Kuchangamkia Fursa Mradi wa Bomba la Mafuta
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo (kulia) akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari na mwongozaji
wa kipindi cha 360 cha Clouds TV, Hassan Ngoma katika mahojiano maalum
kuhusu uzinduzi wa mradi wa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka
Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika
Agosti 05, mwaka huu yaliyofanyika mapema Julai 31, mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
*********
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo amewataka wananchi wanaoishi katika mikoa itakayopitiwa na
miundombinu ya bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini
Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania kuchangamkia fursa
mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
Dkt.
Pallangyo aliyasema hayo Jumatatu jijini Dar es Salaam kupitia kipindi
maalum cha 360 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds wakati
akielezea maandalizi ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta
ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa
kufanyika Agosti 05, mwaka huu.
Alisema
kuwa wananchi katika maeneo husika wanatakiwa kujiandaa kwa ajira
wakati wa maandalizi na utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na utoaji
wa huduma mbalimbali za vyakula, usafiri na ufundi.
“Fursa
zitakazokuwepo ni nyingi mno, vijana waliomaliza Vyuo vya Ufundi
wataweza kufanya kazi za uchomeleaji wa vyuma, madereva wenye leseni
kupata kazi, wakina mama lishe kuuza vyakula, wakulima kuuza mazao kwa
walaji watakaoongezeka kutokana na uwepo wa mradi huo, alisema Dkt. Pallangyo.
Akielezea
manufaa ya mradi huo, Dkt. Pallangyo alieleza kuwa kukamilika kwa mradi
huo kutaleta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi za Uganda na
Tanzania.Alisisitiza kuwa mradi utatoa takribani ajira 10,000 na
kufungua fursa za biashara katika mikoa itakayopitiwa na mradi
“Mradi
utapelekea kufunguka kwa Ukanda wa Biashara kwa nchi nyingine za Afrika
Mashariki kama vile Rwanda, Burundi, Kongo, Sudan ambapo wanaweza
kuunganishwa na miundombinu hiyo na kusafirisha mafuta kwa urahisi,” alisisitiza Dkt. Pallangyo.
Aliendelea
kusema kuwa, kukamilika kwa mradi huo nchi za Tanzania na Uganda
zitapata mapato na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wake.
Dkt.
Pallangyo alieleza faida nyingine kuwa ni pamoja na gharama za mafuta
kupungua kutokana na nchi za Afrika Mashariki kutumia mafuta yake
yenyewe kwenye magari pamoja na ndege hivyo kuchochea kasi ya utalii
katika nchi husika pamoja na ajira.
Awali
akielezea mradi huo, Dkt. Pallangyo alisema kuwa mradi ulikuwa na
ushindani mkubwa hata hivyo bado ilionekana Tanzania kuwa na vigezo vya
bomba hilo kupita katika sehemu kubwa ya ardhi yake ambapo alieleza
vigezo hivyo kuwa ni pamoja na hali ya tambarare katika ardhi ya
Tanzania hivyo gharama za uwekezaji kuwa rahisi.
Aliongeza
kuwa ardhi ya Tanzania ni rahisi pamoja na kuwepo kwa hifadhi ya
barabara katika maeneo mengi hali inayopelekea gharama za fidia kuwa
ndogo.
Dkt.
Pallangyo alieleza vigezo vingine kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa na
uzoefu mkubwa katika usimamizi wa bomba la Mafuta la TAZAMA na la Gesi
linalotoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam.