ACT Wazalendo kudai mikutano ya hadhara mahakamani
Chama
cha ACT-Wazalendo kimepanga kufungua shauri Mahakama Kuu kupinga amri
ya kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa wale ambao hawakushinda
kwenye uchaguzi katika majimbo husika.
Chama hicho kimefikia uamuzi huo kupitia Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa pili uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa
ya mkutano huo iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa chama
hicho kimeamua kufungua shauri hilo kudai haki ya kufanya mikutano ya
hadhara ambayo ni shughuli halali za vyama vyote vya siasa kwa mujibu wa
katiba.
Aidha,
taarifa hiyo imeeleza kuwa mbali na kufungua shauri hilo, wameazimia
kumuandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumuomba atengue zuio la
kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.
“Maazimio
haya yote yatapelekwa kwenye idara husika za chama kwa ajili ya
kutekeleza mara moja. Pia, viongozi wa chama wataendelea kuipigania
misingi ya kidemokrasia,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
ACT
Wazalendo walishinda jimbo moja pekee la ubunge la Kigoma Mjini ambapo
kwa mujibu wa masharti ya kufanya mikutano ya hadhara ndilo jimbo pekee
ambalo chama hicho kinaweza kufanya mkutano wa hadhara wa jimbo.
Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa chama hicho ndiye mbunge pekee anayekiwakilisha bungeni.