Wawili wafariki baada ya daladala kugonga treni Dar
Watu
wawili wamefariki dunia na wengine 36 wamejeruhiwa baada ya gari la
abiria (daladala) kugonga kichwa cha treni katika eneo la Yombo, Temeke
jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kipolisi wa Temeke, Gilles
Moroto (pichani) waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea mapema leo
asubuhi ni mwanamke mmoja aliyekuwa abiria wa gari hilo aina ya coaster
na mwanaume mmoja ambaye ni kondakta.
Kamanda
Moroto amesema kuwa kati ya majeruhi 36 wa ajali hiyo, majeruhi wanne
wako katika hali mahututi na kwamba wote wamepelekwa katika hospitali ya
wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Majeruhi
wote wanapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Temeke. Miongoni
mwa majeruhi hao, wanne wapo katika hali mbaya,” amesema Kamanda
Moroto.
Mashuhuda
wa ajali hiyo wamepongeza juhudi za wananchi kwa ushirikiano wao katika
kusaidia kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo kwa kuwatoa ndani ya gari.