Rais Magufuli: Tukikaza Mkanda Kidogo, Lazima Tutakusanya Kodi ya Trilioni 2 kwa Mwezi
Wakati
takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikionyesha makusanyo ya
kodi kwa mwezi ni wastani wa Sh trilioni moja hadi 1.3, Rais Dk. John
Magufuli, amesema kibano cha kodi kikiongezwa kidogo, mapato yatafika
hadi Sh trilioni mbili kwa mwezi.
Kauli
hiyo aliitoa mjini hapa jana asubuhi, wakati akihutubua wananchi wa
Wilaya Kibonda, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya
Kibondo-Nyakanzi.
“Fedha
zinazofanya miradi ni zenu, Serikali haina shamba, haina chochote,
inategemea kodi za wananchi, ndiyo maana mimi nawachukia sana wanaokwepa
kulipa kodi,” alisema.
Pia
alisema wanaokwepa kulipa kodi si wananchi wa kawaida, bali ni watu
wakubwa kwa sababu wananchi wanalipa hata wanapotoa nauli za basi.
“Mkipanda
kwenye basi, lililipiwa kodi lilivyonunuliwa na mafuta yakiwekwa
mnalipa mkodi, ni jukumu tu la waliokusanya kodi kwenye vituo vya mafuta
wazirudishe Serikalini, lakini wapo wanaobaki nazo. Hao ndio nataka
kulala nao mbele, nimeshatoa siku 14 na sasa hivi zimekabaki 12 au 13,” alisema na kuongeza:
“Serikali
ikikusanya kodi, baadaye inazirudishe kwenye maendeleo ya wananchi,
tulipoingia madarakani kwa awamu ya tano, kodi zilizokuwa zinakusanywa
kwa mwezi ilikuwa kati ya shilingi bilioni 800 hadi 850, tulipobana tu
kidogo, tunakusanya shilingi trilioni 1.2 hadi shilingi trilioni 1.3 kwa
mwezi.
“Nina
uhakika tukibana zaidi tutapata shilingi trilioni mbili ama shilingi
trilioni mbili na kitu, tulipokusanya hizo shilingi trilioni 1.2 hadi
shilingi trilioni 1.3, ndugu zangu wa Kakonko na Watanzania kwa ujumla,
tulianza kuzitumia fedha hizo, tulianza kwa kutoa elimu bure kwa watoto
wetu kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari wanasoma bure, hakuna
kulipa ada.
“Walikuwa wanasoma group (kundi) la watu fulani tu wakubwa, watoto wa masikini hawaendi shule, nikasema haiwezekani.
“Kwenye
kampeni niliwaambia nitasomesha Watanzania bure, wakasema haiwezekani,
nikawaambia nimekuwa waziri kwa miaka 20 najua zinapovuja nitaenda
kuziba hukohuko.”
Alisema fedha nyingi zimekuwa zikivuja serikalini kutokana na matumizi mabaya ndani ya Serikali.
“Watu
wanazunguka wanatembea kila mahali, semina za ajabu ajabu, mikutano ya
ajabu ajabu, posho za ajabu ajabu, hizo ndiyo zimekuwa ni fedha za
wananchi wanyonge. Na mimi nimesema semina hamna, maposho ya ajabu
ajabu hamna, kusafiri hadi nikupe kibali, ili fedha zinazobaki zirudi
kwa wananchi,” alisema.
Alisema
kwa matokeo ya kubana fedha hizo, kwa mwaka huu bajeti ya dawa imepanda
kutoka Sh bilioni 30 hadi Sh bilioni 250 na vitanda vya Sh bilioni 33
vimenunuliwa kwa ajili ya hospitali.