UKARABATI WAPAMBA MOTO UWANJA WA CCM KIRUMBA JIJINI MWANZA
Judith Ferdinand, Mwanza
Uwanja wa Michezo wa CCM Kirumba jijini hapa unaendelea
kufanyiwa ukarabati katika maeneo mbalimbali, ili kukidhi hadhi ya
kimataifa.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM),mkoa wa Mwanza Raymond Mwangwala, wakati akizungumza na
Majira ofisini kwake mkoani hapa.
Mwangwala alisema, ukarabati huo umefanyika katika maeneo
ya msingi ikiwa ni pamoja na upandaji nyasi katikati ya uwanja(Pitch)
ambazo zimegharimu shilingi 711000 na kuzibua mifereji ya kupitisha maji
machafu iliyokuwa imeziba ndani ya uwanja.
Pia wamefanya marekebisho ya magoli kwa kuongeza ukubwa
kama walivyokua wameelekezwa pamoja na kukarabati vyoo sita ambavyo
vimekua na hadhi ya kimataifa ambapo viongozi wa TFF wameisha vikagua na
kuridhishwa navyo.
Hata hivyo alisema,mpaka kufikia tarehe 15 July mwaka
huu,katika mechi ya kirafiki kati ya Rwanda na Tanzania, watakua
wameishakamilisha kufanya marekebisho katika maeneo ya msingi.
Aidha alisema,marekebisho mengine yataendelea kabla ya ligi
kuu kuanza,pia wanatarajia kuongeza taa,ili waweze kupata mechi za
usiku sambamba na kuweka runinga(Television) sehemu mbalimbali ndani ya
uwanja kwa ajili ya mashabiki walio mbali waweze kufuatilia kwa ukaribu
michezo inavyoendelea.
Na wakati huohuo Mwangwala aliwaomba wakazi wa Mwanza na
mikoa jirani kujitokeza kushuhudia na kushangilia timu ya taifa katika
mchezo wa kirafiki unaotarajiwa kutimua vumbi mapema July 15 katika
uwanja wa CCM Kirumba kati ya timu ya taifa ya Rwanda na Taifa Stars.
Vilevile alisema, wanataka kuutangaza uwanja huo pamoja
na mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa kituo cha michezo katika nchi za
Afrika Mashariki.