AGPAHI YAKUTANA NA WAGANGA WAKUU WA MIKOA MJINI DODOMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akizungumza wakati wa mkutano wa waganga wakuu wa mikoa ambako shirika hilo linafanya kazi nchini Tanzania. 
Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi nchini Tanzania limekutana na waganga wakuu wa mikoa saba ambako linatekeleza shughuli zake. 

AGPAHI imefanya mkutano na waganga wakuu wa mikoa ya Shinyanga,Mwanza,Geita,Simiyu,Tanga,Mara na Manyara siku ya Jumatano, Julai 5,2017 katika ukumbi wa Morena Hotel mjini Dodoma. 

Akizungumza katika mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema lengo ni kujadiliana kuhusu maendeleo, mafanikio na changamoto za miradi na kupanga mikakati ya utekelezaji wa miradi katika mwaka ujao wa miradi.

Dk. Mwakyusa alisema lengo la AGPAHI ni kuboresha afya ya watoto na familia kwa kutokomeza VVU na Ukimwi na kutoa huduma za kinga,matunzo na tiba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya ikiwemo serikali ili kubuni na kutekeleza mikakati muafaka kwa afya bora.

“Shirika hili lilianzishwa mwaka 2011,kuanzia kipindi hicho tulikuwa tunafanya kazi zetu katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, lakini kuanzia Oktoba 2016 mikoa ya Mara,Geita,Tanga na Mwanza iliongezeka (tukitekeleza miradi ya Ukimwi) na mkoa wa Manyara uliongezeka ambako tunatekeleza  mradi wa kifua kikuu”,alisema Dk. Mwakyusa. 

“Tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa kushirikiana kwa ukaribu kabisa na serikali. Na wafadhili wetu wakuu ni Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU kwa hisani ya Watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP – Mozambique)”, aliongeza Dk. Mwakyusa. 

Aidha alisema mbali na mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi pia shirika hilo linatekeleza mradi wa kifua kikuu migodini kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu kifua kikuu kwa wachimbaji, familia zao na jamii inayowazunguka ili waweze kuchukua hatua za haraka kujikinga na kupata tiba sahihi ya kifua kikuu. 

“Mradi huu hivi sasa unatekelezwa katika machimbo ya Iyenze na Mwime halmashauri ya Mji wa Kahama, Kakola na Mwazimba halmashauri ya Msalala katika mkoa wa Shinyanga pamoja na Mererani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ”,aliongeza Dk. Mwakyusa.

Kwa upande wao waganga wakuu wa mikoa hiyo saba walilishukuru shirika hilo kwa jitihada zake za kujali afya za watanzania na kuahidi kuendelea kushirikiana na AGPAHI ili wananchi waweze kunufaika kupitia shirika hilo. 

Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita aliuhakikishia uongozi wa shirika hilo kuwa watakuwa wasimamizi wazuri wa fedha zinazotolewa na AGPAHI ili kutekeleza miradi iliyoanzishwa kwa faida ya watanzania. 

“Kwanza nilipongeze shirika hili kwa kuongeza mikoa lakini pia kuamua kutukutanisha hapa, kwa kweli huu ni utaratibu mzuri na naomba tuendelee kushirikiana, sisi tupo tayari kuhakikisha tunasimamia miradi iweze kutekelezeka”, aliongeza Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume. 

Shirika la AGPAHI linajishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kutoa huduma ya uchunguzi na huduma za awali ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango, pia shirika hutoa vifaa tiba, kukarabati miundombinu ya vituo vya afya, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kwa msaada wa watu wa marekani. 
Meneja Mawasiliano kutoka AGPAHI, Jane Shuma akiwakaribisha waganga wakuu wa mikoa katika ukumbi wa Morena Hotel mjini Dodoma kwa ajili ya kushiriki mkutano ulioandaliwa na shirika hilo. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akielezea kuhusu miradi ya Ukimwi inayotekelezwa na shirika hilo katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania. 
Waganga wakuu wa mikoa saba wakimsikiliza Dk. Mwakyusa. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akizungumza ukumbini.Kushoto ni Mkurugenzi wa Miradi kutoka shirika la AGPAHI, Dk. Safila Telatela. 
Dk. Mwakyusa akiendelea kuelezea kuhusu miradi inayotekelezwa na shirika la AGPAHI nchini Tanzania. 
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume( kulia) na Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk. Sungwa Kabissi wakimsikiliza Dk. Mwakyusa. Mkutano ukiendelea.
Dk. Mwakyusa akielezea jinsi ambavyo shirika hilo lilivyojipanga kuhakikisha kuwa watanzania wengi wananufaika na huduma zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akiwasilisha mada kuhusu mradi wa kifua kikuu migodini unaotekelezwa na shirika hilo katika halmashauri za wilaya za Kahama Mji na Msalala mkoani Shinyanga na wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara. 
Kaimu Mganga mkuu mkoa wa Simiyu, Dk. Chacha Magige (kushoto) na Mganga mkuu mkoa wa Mara, Dk. Francis Mwanisi (kulia) wakisoma taarifa mbalimbali zilizotolewa na shirika la AGPAHI kwa kila mkoa ambako shirika hilo linafanya kazi zake. 
Waganga wakuu wa mikoa wakisoma taarifa za masuala ya VVU na Ukimwi zilizotolewa na shirika la AGPAHI. Katikati ni Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Dk. Leonard Subi. Kulia ni Kaimu Mganga mkuu mkoa wa Simiyu, Dk. Chacha Magige .Wa kwanza kushoto ni Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga Dk. Asha Mahita. 
Mganga mkuu mkoa wa Mara, Dk. Francis Mwanisi akichangia hoja wakati wa mkutano huo. 
Meneja Ruzuku kutoka AGPAHI, Umboke Mwakilima akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya fedha za miradi inayotekelezwa na shirika hilo. 
Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita (katikati) akichangia hoja wakati wa mkutano huo. Kulia ni Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Dk. Leonard Subi, kushoto ni Mganga mkuu mkoa wa Geita, Dk. Joseph Kisala.
Dk. Mahita akisisitiza jambo ukumbini.
Dk. Leonard Subi akichangia hoja ukumbini.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk. Sungwa Kabissi akichangia hoja wakati wa mkutano huo. 
Mganga mkuu mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume akizungumza ukumbini. 
Mkurugenzi wa Miradi kutoka shirika la AGPAHI, Dk. Safila Telatela akiwasisitiza waganga wakuu wa mikoa kushirikiana na AGPAHI katika kufanikisha miradi ya masuala ya afya.
 Dk. Telatela akisisitiza jambo ukumbini.
Picha ya pamoja: Viongozi wa shirika la AGPAHI na waganga wakuu wa mikoa ambako shirika hilo linafanya kazi zake. 
Picha ya pamoja: Viongozi wa shirika la AGPAHI na waganga wakuu wa mikoa. 

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Powered by Blogger.