RAIS MAGUFULI AMMWAGIA SIFA KAFULILA ADAI WALIOMWITA TUMBILI SAKATA LA IPTL WAO NDIYO MATUMBILI
Rais wa Jamuhuri wa Muungano Wa
Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amempongeza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
la Kigoma Kusini, David Kafulila kutokana na namna alivyojitoa katika
kutetea maslahi ya Watanzania kwenye sakata la Escrow(IPTL) na kuonesha
uzalendo mkubwa ambao hawezi kusahaulika katika historia ya Tanzania.
Rais Magufuli ameyasema hayo alipokuwa
akizungumza na wakazi wa Kata ya Nguruka katika hafla ya uzinduzi wa
mradi mkubwa wa maji uliopo Tarafa ya Nguruka katika Wilayani Uvinza
ambapo alisema kuwa akiondoka hapo bila kumpongeza Kafulila atakuwa
amefanya dhambi ya unafiki itakayompeleka motoni.
Akizungumza, Rais alisema anatambua
kwamba Kafulila yupo chama kingine, lakini kwenye suala la IPTL, aliweka
maslahi ya Taifa mbele na kusimamia ukweli hivyo anampongeza na pongezi
hizo ni za dhati kwani zinatoka moyo. Rais alieleza umma uliokuwa
umejitokeza mahali hapo kuwa, wizi uliokuwa unafanywa na IPTL ni mkubwa
hivyo Kafulila alisimama kutetea umma wa watannzani.
Lakini pia Rais alieleza vikazwo ambavyo
Kafuli alikutana navyo wakati akipambana kuhusu wizi huo uliokuwa
ukiratibiwa na baadhi ya watumishi wa serikali kwa manufaa yao wenyewe.
“Wakamtisha wengine kumpeleka
mahakamani, wakamtukana wee, wengine wakamuita tumbili, sasa tumbili
amefanya makubwa kwa ajili ya Watanzania. Wao ndio matumbili, huyu
(Kafulila) alifanya kazi ya Mungu ya kuwatumikia Watanzana,” alisema
Rais Magufuli huku wakazi wa eneo hilo wakilipuka kwa furaha.
Akiendelea kumwaga sifa hizo za dhati,
Rais Magufuli alisema kwenye hili suala la wizi wa IPTL, atampongeza
Kafulila kwa maisha yake yote.
Akizungumzia suala la uzalendo, Rais
amesema nchi ilikosa uzalendo na kwamba kila aliyekuwa akichaguliwa
alikazana kukusanya mali zake yeye mwenyewe bila kujua kuwa atakufa na
atazikwa kwenye shimo moja, hivyo akawasihi watanzania wajenge uzalendo.
Alisema maendeleo hayana chama na
kwamba, kiongozi mzuri ni yule anayewatumikia watu wake bila kujali
chama, kwani mradi huo wa maji anaoufungua utanufaisha watu wote hata
wasio na chama. Alieleza kwamba, ushabikia wa vyama ndio unaochelewesha
maendeleo ya watanzania.
Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya
kikazi ya siku tatu Mkoani Kigoma kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi
wa Maji mkubwa katika kata ya Nguruka uliogharimu zaidi ya shilingi
bilioni 2 ambao unatarajiwa kukamilika Disemba 30 mwaka huu ambao
utafuta kero ya maji kwa wananchi wa kata ya Nguruka.