MKURUGENZI WA HALMASHAURI ATUMBULIWA KWA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA UMMA
Katika
kuhakikisha kunakuwepo na matumizi mazuri ya fedha za umma, Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa
wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa hao mapema hii leo wakati
alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye
ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Amesema kuwa Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya
Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na
wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
“Halmashauri inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona
Halmashauri hii na zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali
hii no, hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi.”amesema Majaliwa
Aidha, amesema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa
dhamana wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi
wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za
maji, afya na elimu, hivyo itaendelea kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, Majaliwa amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika
Halmashauri zote nchini wabadilike na wahakikisha wanashirikiana na
kufanya kazi kwa ushirikiano kwani wakigawanyika watashindwa kutekeleza
majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.