Rais Magufuli Amenza Ziara Mkoani Tabora Na Kuzindua Miradi Ya Barabara
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 23 Julai, 2017 ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Nguruka
uliopo katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kufungua miradi miwili
ya barabara za Kaliua – Kazilambwa na barabara ya Tabora – Ndono –
Urambo.
Mradi
wa Maji wa Nguruka ambao utakamilika tarehe 31 Desemba, 2017 utagharimu
Shilingi Bilioni 2.87 na ni miongoni mwa miradi 1,810 ya maji
inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za mfuko wa maji nchi nzima
ambapo mpaka sasa miradi 1,333 kati yake imekamilika na miradi 477 ipo
katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Barabara
ya Kaliua – Kazilambwa ina urefu wa kilometa 56 imejengwa kwa gharama
ya Shilingi Bilioni 61.86 na barabara ya Tabora – Ndono – Urambo yenye
urefu wa kilometa 94 imejengwa gharama ya Shilingi Bilioni 118.96, fedha
za miradi yote miwili zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza
na wananchi katika sherehe za miradi hiyo pamoja na wananchi waliokuwa
wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Uvinza, Mpeta, Usinge,
Isawima, Igagala, Ndono, Kalola na Ilolangulu, Mhe. Rais Magufuli
aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli alimuagiza Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kuhakikisha barabara
za Urambo – Kaliua yenye urefu wa kilometa 28 inaanza kujengwa ndani ya
mwezi mmoja na barabara ya Nyahua – Chaya yenye urefu wa kilometa 85
inaanza kujengwa ndani ya mwezi mmoja na nusu kwa kiwango cha lami.
Mhe.
Rais Magufuli pia amewahakikishia wananchi wa Uvinza kuwa Serikali
imeshapata fedha za kujenga barabara ya Uvinza – Malagarasi yenye urefu
wa kilometa 50 na amemuagiza Waziri Mbarawa kuanza maandalizi ya ujenzi
wa barabara ya Kazilambwa – Chagu yenye urefu wa kilometa 41.
Mhe.
Rais Magufuli alisema Serikali imeweza kutekeleza miradi hiyo kwa fedha
zake inazozipata kutokana na makusanyo ya kodi hivyo amewataka
Watanzania kuhakikisha wanalipa kodi ipasavyo na wanadai risiti kila
wanaponunua bidhaa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kukabiliana na mianya yote ya upotevu na matumizi mabaya ya fedha za
Serikali.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuhifadhi mazingira kwa
kujiepusha na vitendo vya ukataji miti katika maeneo ya hifadhi na
kupunguza idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa maeneo ya malisho
waliyonayo na amekataa ombi la wananchi wa Kijiji cha Isawima waliotaka
kuongezewa eneo la Kijiji hicho kwa kilometa 20 zaidi kuingia hifadhini.
Kuhusu
tatizo la soko la tumbaku linalowakabili wakulima wa zao hilo mkoani
Tabora Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wakulima kuwa na subira kwa kuwa
Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa imeanza
kushughulikia tatizo hilo.
Katika
ziara ya hiyo Mhe. Rais Magufuli aliongozana na Mawaziri wawili Prof.
Makame Mbarawa Mnyaa na Prof. Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Daniel Nzanzugwanko na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman
Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambao wamempongeza kwa kazi
nzuri inayofanywa na Serikali na wamesema wanaunga mkono juhudi hizo.
Leo
tarehe 24 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa
Tabora ambapo ataweka jiwe la msingi la mradi wa maji kutoka ziwa
Victoria, atafungua mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora eneo
la Kaze-Hill, atafungua barabara za Tabora – Nyahua na Tabora – Nzega na
atazungumza na wananchi katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mjini
Tabora.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tabora