Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
MTENDAJI wa Mtaa Mondo kata ya
Guduwi, halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu amejikusanyia zaidi ya
shilingi 300,000/= kwa njia ya udanganyifu kupitia Tangazo la serikali
liliowataka vijana waliohitimu kidato cha nne kuomba nafasi za uhudumu wa
afya ngazi ya vijiji.
Kufuatia Tangazo toka wizara ya
afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto wametangaza nafasi za masomo
ya uhudumu wa afya ngazi ya jamii kwa mwaka 2017/18 likiwataka vijana
waliohitmu kidato cha nne na ufaulu wa masomo 4 kwa wastani wa D huku somo la
Biology likipewa kipaumbele.
Inadaiwa kuwa Mtendaji huyo Fred
Joseph amekuwa akiwatoza fedha vijana hao ili kuwasaidia juu ya kufanya maombi
ya nafasi hizo wakati tangazo liliwataka kulipia elfu 30,000/= kwa ajili ya
udahili wa Nacte.
Wakiongea kwa nyakati tofauti na
waandishi wa Habari vijana hao walisema kuwa baada ya kusomewa Tangazo hilo na
sifa zake, walipomfuata mtendaji kwa ajili ya kuwaidhinisha anawaomba fedha
akidai kuwa atawasadia kutuma maombi yao na kuhakikisha wanapata nafasi.
‘’kila aliyekidhi sifa za uombaji
akienda kwa mtendaji anaombwa fedha…akikosea haidhinishiwi, hivyo kulingana na
hali tuliyonayo tunawaomba wazazi fedha na kumpa tukijua ni maelekezo toka
wizara ya afya’’ alisema mmoja wa Vijana ambaye jina linahifadhiwa.
Aliongeza kuwa kuna vijana wawili
kila mmoja ametoa laki mojamoja, wengine wawili na yeye akiwemo wametoa
shilingi elfu 50,000/= kila mmoja na kijana mmoja ametoa shilingi elfu
30,000/=.
Mratibu wa zoezi hilo toka kituo cha
Afya Muungano Yustina Sweya alisema kuwa baada ya kupokea Tangazo hilo toka
Wizarani walilipeleka kwa wananchi kama lilivyo ili atakayekidhi vigezo atume
maombi kwa gharama ya shilingi elfu 30 tu.
Aliongeza kuwa mtedaji huyo anafanya
makosa kuwaomba fedha vijana hao kwa ajili ya kuwaidhinisha kwa kuwa hayo ni
moja ya majukumu yake na wao hawajaaagiza kutoza vijana hao fedha yoyote.
Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya
mji wa Bariadi Akilimali Mpozemenya alisema kuwa kufuatia Tangazo hilo
hawajaagiza vijana kutozwa fedha na kuhakikisha kuwa watamkata mtendaji huyo
anayeidharirisha wizara kwa kuwa haikutoa maelekezo kama hayo.
‘’hii ni fedheha kwa wizara ya afya
inayofanywa na baadhi ya watumishi katika maeneo yao sisi hatujaagiza
kufanyika, nadhani tangazo linajitosheleza katika maelekezo yake…hivyo
tutahakikisha mtendaji huyo anakamatwa kwa sababu anawaibia vijana wetu’’
alisema Mpozemenya.
Kwa upande wake Fred Joseph
alisema kuwa yeye ni mtendaji wa mtaa wa Mondo na amekuwa akikaimu mtaa wa
Guduwi mbugani hivyo hajawahi kuomba fedha na badala yake wajumbe wa serikali
ya mtaa wakati wa kupitisha majina hayo wanawaomba fedha ya maji kwa vijana hao
kwa sasabu wamepata nafasi hizo bure.
Aliongeza kuwa hadi sasa wamepitisha
vijana wanane na yeye kama kiongozi hahusiki na kuongeza kuwa wajumbe wake
ndiyo wamekuwa wakiwaomba fedha vijana hao na yeye akipatia kidogo kutokana na
kufanya uhamasishaji ili wajitokeze kwa wingi.
‘’mondo kuna vjiana wanne, mbugani
wapo wanne, nafanya uhamasishaji ili vijana wajitokeze kwa wingi, nawaandikia
barua ya kuwaidhinisha, nawaandikia muhtasari karatasi tano pia naambatanisha
na vivuli vya vyeti vyao ili kuwasaidia…mimi sijawahi kuwaomba fedha isipokuwa
wajumbe wangu wanaomba pindi tunapokuwa tunapitisha majina’’ alisema Fred.
Alisema kuwa hata yeye ameshasikia
tuhuma hizo juu ya vijana hao kutozwa fedha, lakini amekuwa wakiwashauri
wajumbe wake wasiwatoze kiwango kikubwa cha fedha kisichozidi elfu 50,000/= ili
30,000/= itumike kufanya maombi na inayobaki wagawane.
Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kupitia ofisi ya Mganga mkuu wa Halmashauri ya mji wa
Bariadi imetangazia nafasi za masomo ya uhudumu wa afya ngazi ya vijiji kwa
vijana waliohitumu kidato cha nne au cha sita ili baada ya kuhitimu mafunzo
hayo waweze kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo ya vijijini na kupunguza
changamoto ya uhaba wa watumishi wizara ya afya.
|