Kubenea Aitwa Polisi Akidaiwa Kumtisha Profesa Lipumba
Mbunge
wa jimbo Ubungo,(CHADEMA) Saed Kubenea ameitwa polisi na kutakiwa
kuripoti leo tarehe 20/7/ 2017 kutoa maelezo kituo cha polisi kufuatia
malalamiko aliyotoa Profesa Lipumba Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Mbunge
wa Ubungo Mh Saed Kubenea wiki iliyopita alifanya mkutano na vyombo vya
habari kama Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani akiwa pamoja na baadhi ya
viongozi wa CUF iliyochini ya uongozi wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
na kutangaza oparesheni ya kumuondoa Profesa Lipumba katika ofisi za
chama cha CUF Buguruni.
Baada
ya Kubenea kutangaza oparesheni hiyo siku mbili mbele aliibuka Profesa
Lipumba na kwenda kituo cha polisi kutoa malalamiko juu ya kile
alichokisikia kutoka kwa kiongozi huyo na oparesheni hiyo aliyotangaza.
"Ni
kweli Kubenea ameitwa na kuitwa kwake kumekuja baada ya wiki iliyopita
kufanya mkutano na waandishi wa habari kama Makamu Mwenyekiti wa Kanda
ya Pwani akiwa pamoja na viongozi wa CUF inayoongozwa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro na Katibu Mkuu Maalim Seif na
kutangaza operesheni inayoitwa 'Operesheni Ondoa Msaliti Buguruni (OMB).
Operesheni hiyo itaendeshwa kwa ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA" ilisema taarifa ya CHADEMA
Profesa
Lipumba na baadhi ya viongozi wa CUF wapo katika mgogoro kutokana na
kiongozi huyo kipindi cha uchaguzi mwaka 2015 kuandika barua ya
kujiuzulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa CUF taifa na kubaki mwanachama
wa kawaida, lakini baada ya uchaguzi kupita kiongozi huyo akataka
kubatilisha maamuzi yake ya kujiuzulu jambo ambalo viongozi wa CUF na
baadhi ya wanachama wamekuwa wakilipinga na kukataa, japo Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi yeye bado anamtambua
Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF taifa.