MPANGO WA CCM KUGAWA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU WATILIWA SHAKA

Mpango wa CCM wa kutaka kusaidia wanafunzi yatima, walemavu na wenye wazazi wasiojiweza ambao walikosa mikopo kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu, umeibua maswali.


Maswali hayo yameibuka baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wanafunzi wenye matatizo hayo wafike ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM iliyopo Mtaa wa Lumumba jijini hapa.

Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), watu saba kati ya kumi walioomba mikopo kwa mwaka 2016/17, hawakupata, hali ambayo imefanya wadau mbalimbali kutaka hatua zichukuliwe kusaidia wengi zaidi.

Kilio hicho kimeifanya CCM itangaze mpango huo wa kusaidia waliokosa mikopo, ikiweka vigezo vya ulemavu, wenye wazazi wasiojiweza na yatima.

Hata hivyo, mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema hiyo ni tabia ya CCM kujijenga kichama kupitia mapengo ambayo kimsingi yametengenezwa na Serikali yake.

Alisema suala la mikopo ni wajibu wa Serikali, hivyo kuwapo kwa wanafunzi walioikosa, tena wenye mahitaji maalumu kama hao, kunaonyesha haikutimiza wajibu wake.

“Utaratibu huu unaidhalilisha Serikali kwa kuonyesha kuwa ni dhaifu na mambo muhimu kama ya kutoa elimu yanayotakiwa kufanywa nayo, yanafaanywa na chama,” alisema Mnyika.

“Ipo haja ya kuhoji kodi za wananchi zinafanya nini kama wao wameshindwa kuzitumia ipasavyo na kukiachia chama kufanya hivyo,” alisema Mnyika.

Mbunge huyo alisema ipo haja kwa Waziri wa Elimu kuliona hilo kama kashfa upande wake kwa sababu ameshindwa kusimamia kazi zake na kumuachia mtu mwingine kufanya hivyo.

Hoja kama hiyo alikuwa nayo Benjamini Nkonya, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirikisho la watoaji elimu wasiotegemea bajeti ya Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (Ciepssa).

“Kinachofanyika ni sawa na kupulizia manukato uvundo badala ya kuangalia namna ya kuuondoa,” alisema Nkonya.

Alisema kwa miaka mingi wamekuwa wakipigia kelele wanafunzi kupewa mikopo bila kujadili shule walizosoma kwa sababu kuna ambao wanasomeshwa kwa ufadhili na unapofika wakati wa kupata mikopo ya elimu ya juu huachwa kwa kisingizio cha kuwa na uwezo.

Nkonya alisema mwaka 2013 kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) uliofanyika Mbeya, walimueleza mgeni rasmi ambaye alikuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa madhara ya upimaji huo wa wanafunzi wanaostahili kupata mikopo.

Mkurugenzi huyo alisema wakati huo shirikisho lao lilikuwa na shule na vyuo 3,400 binafsi nchi nzima na kwa hesabu ya haraka kila taasisi ilikuwa na yatima sita inaowasomesha bure, lakini hawakuweza kupata mikopo kwa hoja kuwa walisoma shule za kulipia.

“Asipake manukato uvundo, suala hili liingizwe kwenye mijadala ya Serikali ili lijadiliwe ikiwa ni pamoja na kushirikisha Tamongsco ambao alisema wapo tayari.

“Bodi ya mikopo katika vigezo ilivyotaja mwaka wa masomo 2016/17 ni pamoja na kuwapa nafasi yatima na wasiojiweza. Kama wapo ambao hawakupata wanaojiorodhesha leo kwa ajili ya kupewa na CCM, bila shaka kuna mahali hapakuwa sawa, ” alisema Nkonya.

Aliishauri Serikali ifanye kama Kenya ilivyofanya kwa kusajili yatima wote na kuwafuatilia popote walipo ili kuepuka mkanganyiko.

Stanslaus Kadugazile, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), alipongeza hatua hiyo ya CCM, akisema kama hawajabagua wanafunzi wanaotaka kuwasaidia kwa itikadi za chama wamefanya jambo la busara.

Pia, msomi mmoja ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini kwa kile alichodai ni mjadala dhaifu, alisema jambo hilo lina maswali mengi kuliko majibu.

Alisema mpango wa CCM haujaeleza kama ni wa nchi nzima au Dar es Salaam pekee, kwa sababu unapozungumzia walemavu moja kwa moja umezungumzia uwakilishi badala ya kila mmoja kufika wenyewe.

“Unaratibiwa na nani, fedha zimetoka katika mpango upi wa chama? Anapimaje yatima na kujiridhisha kuwa wanahitaji msaada huo? Kwa sababu wapo yatima matajiri waliorithi mali kwa wazazi wao,” alisema msomi huyo.

Alisema kutoa elimu si jambo la dharura, bali linahitaji mipango tena endelevu kama ilivyo kwa ulinzi wa nchi na suala la hali ya chakula. Kwa misingi hiyo, alisema mpango huo unahitaji kuangaliwa upya.

Wakati huohuo, Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM imesema wameshapokea wanafunzi 20.

Mbali na mikopo kwa wanafunzi, CCM imekuwa ikihamasisha wanachama wake kujikusanya katika vikundi vya watu wanne ili kiwawezesha kupata mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vijana na wanawake.

Uchunguzi wa gazeti la  Mwananchi ulibaini kuwa katika baadhi ya halmashauri, vijana hutakiwa kukata kadi ya CCM kwanza, jambo ambalo limefanya mikopo hiyo ipewe jina la “mikopo ya CCM”.
Powered by Blogger.