IGP SIRRO: TUTAENDELEA KUWAKAMATA WANASIASA WACHOCHEZI
Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro amefunguka na
kusema kuwa jeshi la polisi nchini litaendelea kuwakamata na
kuwachukulia hatua mbalimbali baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa
nchini wenye lengo la kufanya uchochezi.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya jeshi la polisi nchini
kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu ambaye pia
ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kutuhumiwa kutoa
maneno ya kichochezi.
Aidha Sirro amedai kuwa jeshi hilo litaendelea kuwachukulia hatua kali
za kisheria ambazo ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani viongozi wa vyama
vya siasa wanaojaribu kujitafutia umaarufu kwa kutoa kauli zenye utata
hasa zile zinazolenga kuchochea vurugu jambo linaloweza kusababisha hali
ya uvunjifu wa amani ambayo imedumu hapa nchini kwa muda mrefu.
Viongozi wa CHADEMA ndiyo wamekuwa wahanga namba moja kukamatwa na jeshi
la polisi nchini kwa tuhuma za kutoa lugha za kuudhi, na uchochezi
ambapo kwa mwezi huu wa saba pekee zaidi ya viongozi 10 wamekamatwa na
jeshi la polisi kwa makosa mbalimbali.