GARI LATUMBUKIA MTO WAMI NA KUUA WATU WAWILI
Picha hii ya mtandao inaonyesha moja ya ajali zilizowahi kutokea katika mto huo.
MADEREVA
wawili wa kampuni ya Usangu Logistics wamekufa baada ya gari la mizigo
walilokuwa wakisafi ri nalo kutumbukia katika Mto Wami uliopo Chalinze,
wilayani Bagamoyo.
Akizungumza
jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana alisema
ajali hiyo ilitokea usiku wa saa 7:00 kuamkia jana. Gari aina ya Scania
lenye namba za usajili T857 ARP lililokuwa linatoka Dar es Salaam
kwenda Arusha lilikatika breki na kugonga kingo za mto na kutumbukia
mtoni.
Dereva
aliyekuwa anaendesha gari hadi linatumbukia mtoni ametajwa kuwa ni
Yahaya Karim anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35.
Alisema jina na mtu mwingine ambaye pia ni dereva, halikufahamika mara
moja.
Matukio
ya ajali yamekuwa mengi nchini. Kwa mujibu wa jeshi la polisi kitengo
cha usalama barabarani, hadi Novemba mwaka jana watanzania 2,994
walikufa kwa ajali mbalimbali za barabarani za mabasi, malori, magari
madogo, bajaji na bodaboda.
Ili
kukabiliana na ajali hizo, jeshi hilo limekuwa likiendesha operesheni
katika barabara zote kuu nchini kwa mfano kutumia tochi kukamata
madereva wanaoendesha kwa mwendokasi au kwa uzembe.
Pia
limekuwa likiwataka wananchi kushirikiana na polisi kuchukua hatua
mbalimbali za kudhibiti ajali kwa mfano kutoa taarifa mara kwa mara
wakiwa safarini, wanapobaini madereva wanaovunja sheria za usalama
barabarani. Aidha limekuwa likihimiza wananchi kutoa ripoti katika vituo
vya polisi juu ya madereva wanaofanya makosa.
IMEANDIKWA NA JOHN GAGARINI, KIBAHA