KIJANA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KULAWITI WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI


HALID Mohamed (28) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga kwa tuhuma ya kulawiti wanafunzi wawili wa shule ya msingi Chipukizi wilayani Igunga mkoani Tabora.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba aliiambia mahakama mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ajali Milanzi kuwa shitaka la kwanza linalomkabili mshitakiwa huyo lilitokea kati ya Februari 1 mpaka 14 mwaka huu.

Alisema katika Mtaa wa Uarabuni mjini Igunga mshitakiwa alimlawiti mwanafunzi mwenye miaka 9 wa kiume anayesoma darasa la pili shule ya msingi Chipukizi na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.

Aliongeza kwamba shitaka la pili lilitendeka kati ya Februari 1 hadi 14 vilevile katika mtaa huohuo ambapo mshitakiwa alimlawiti mwanafunzi wa miaka 7 wa kiume anayesoma darasa la pili katika shule hiyo hiyo ya Chipukizi.

Alisema mshitakiwa alitenda makosa hayo mawili kinyume na kifungu 154 kidogo cha kwanza (a) (2) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Baada ya kusomewa makosa hayo mawili mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo yote mawili ambapo yuko nje kwa dhamana ya Sh milioni 4 kwa makosa yote mawili na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 17 mwaka huu wakati kesi itakapoanza kusikilizwa

IMEANDIKWA NA LUCAS RAPHAEL,- HABARILEO -IGUNGA
Powered by Blogger.