KAMPUNI ZA SIMU ZAINGIA MATATANI TANZANIA, TCRA YATISHIA KUZIFUTIA LESENI
MAMLAKA ya Mawasilianio Tanzania (TCRA) imeamuru kampuni zote za simu za
mkononi zinazofanya kazi nchini, kusitisha mara moja kutoa matangazo
kwenye huduma za mawasiliano kwani ni kinyume cha Kanuni za Huduma za
Ziada na Kinga ya Mlaji za Mwaka 2015 na 2011, na atakayekaidi atafutiwa
leseni.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alitoa agizo hilo jana Dar es
Salaam baada ya kukutana na wawakilishi wa kampuni za simu za mkononi
kutokana na kuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa huduma,
zinazotolewa na kampuni hizo juu ya matangazo hayo, yanatolewa kabla ya
mpigaji simu kuunganishwa.
Kilaba alisema hatua ya zuio la matangazo hayo kabla ya simu ya mteja
kuunganishwa, linatokana na mamlaka hiyo kujiridhisha kuwa watoa huduma
wengi wa mawasiliano ya simu za mkononi nchini, wamekuwa wakikiuka
vigezo na masharti kama yanavyoelekezwa katika kanuni za huduma za
ziada.
Hivyo, mamlaka imezuia kampuni hizo kusitisha mara moja utoaji wa
matangazo hayo kuanzia jana Julai 6, 2017 ili kuondoa kero. Mtoa huduma
yeyote ambaye atakiuka agizo hilo, atakabiliwa na adhabu kadhaa ikiwemo
kufutiwa leseni ya kuendesha biashara ya utoaji wa huduma za mawasiliano
nchini.
Via>>Habarileo