Jeshi la Polisi Laua Wahalifu Wawili Kibiti

Jeshi la Polisi nchini limewaua watu wawili wanaodaiwa kufanya mauaji katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, mkoani Pwani.

Akielezea tukio hilo jana (Alhamisi Julai 6) ,   Mkuu wa Operesheni Maalumu  za Jeshi la Polisi,  Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilitokea Jumatano  saa nne usiku  katika msitu wa Ngomboroni Kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri.

Wahalifu hao waliuawa na askari wa operesheni maalumu wakiwa katika doria za ufuatiliaji wahalifu sugu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea katika kanda hiyo ya kipolisi.

Alisema askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja muhimu anayeshiriki katika mauaji hayo  ambaye alikamatwa, alikubali kwenda kuwaonyesha polisi mahali  ambapo ni maficho ya wenzake.

“Baada ya kufika  eneo la msitu wa Ngomboroni  kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka  kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika  mashambulizi hayo  mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi  naye alijaribu kutoroka  na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili,” alisema.

Aliongeza; “majeruhi hao wawili  walifariki dunia njiani wakati wakipelekwa hospitali  kwa matibabu kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha ya risasi waliyoyapata. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”

Kamishna Sabas alisema katika tukio hilo wamefanikiwa kupokonya silaha mbili  aina ya SMG  na Shotgun moja pamoja na  risasi tisa.

Kamishina Sabas  amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa wahalifu wengine waliosalia  na kwamba zawadi nono bado ipo pale pale  na itatolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusiana na wahalifu  wanaojihusisha na mauaji katika kanda maalumu ya Rufiji.
Powered by Blogger.