Jeshi la Polisi Dar Latoa Siku 7 Majambazi Wajisalimishe
Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa siku saba kwa
majambazi wote waliowahi kutumikia vifungo na kuachiwa kwa kumaliza
vifungo au rufaa, wajisalimishe kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu.
Kauli
hiyo ilitolewa jijini hapa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu,
Lucas Mkondya wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mkondya
alisema lengo la kuwaita majambazi hao ni kutaka kupanga utaratibu
mzuri ili waone kama baada ya vifungo vyao, wamebadilika na
wanajihusisha na shughuli gani kwa sababu walikuwa ni majambazi sugu na
walifanya matukio.
“Kuanzia
leo (jana) nataka wajisalimishe, wasipojisalimisha wanajua jinsi
tunavyowatafuta kwa sababu ni jambazi hatumtafuti kwa kucheka
tunamtafuta kwa silaha lengo la kuhakikisha hatusikii milio ya bunduki
ikipigwa Dar es Salaam,” alisema Mkondya.
Aidha,
Mkondya aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa, kutoa taarifa kama
kuna majambazi katika maeneo yao ambao wamechiwa ili polisi wawafuatilie
kikamilifu. Katika tukio jingine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 44
wa wizi wa vifaa vya magari pamoja na vifaa hivyo vya magari.
Alisema
watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na operesheni maalumu, ambayo
inalenga kuwakamata wezi wa vifaa mbalimbali vya magari, ikiwa ni pamoja
na wanunuzi wa vifaa hivyo katika sehemu mbalimbali za jiji hili.
Aliongeza
kuwa operesheni hiyo iliyoanza Julai 18, mwaka huu na katika operesheni
hiyo ambayo endelevu, watuhumiwa hao walikamatwa na baada ya kupekuliwa
katika maduka yao walikutwa na vifaa mbalimbali vya magari.
Katika
mahojiano na watuhumiwa wote waliokamatwa, wapo walioshindwa kuvitolea
maelezo vifaa hivyo ni namna gani na wapi vifaa hivyo wamevipata huku
baadhi ya vifaa vikionesha kuwa vimefunguliwa kutoka kwenye magari
mengine kwani vimekutwa na namba za magari.
“Watuhumiwa
wote bado wanaendelea na mahojiano na uchunguzi bado unaendelea ili
kubaini mtandao wote unaojihusisha na wizi huo wa vifaa vya magari ikiwa
ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi,” alisema Kaimu Kamanda.
Aidha,
jeshi hilo linawashukuru wananchi kwa kutoa taarifa na kuwataka
wafanyabiashara wa vifaa vya magari kufuata sheria zinazowawezesha
kufanya biashara hiyo kihalali.
Wakati
huo huo, jeshi hilo limekamata bastola moja aina ya Browning Patent
ikiwa na risasi tisa baada ya majibizano ya risasi kati ya askari polisi
na jambazi mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Adam, ambaye alifariki
dunia katika majibizano hayo.
Alisema
tukio hilo ni la Julai 19, mwaka huu maeneo ya Ubungo Mawasiliano,
ambako awali jambazi huyo na wenzake ambao wanaendelea kutafutwa,
walishiriki katika tukio la mauaji lililotokea maeneo ya Kinondoni Block
41 ambako mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi.
Baada
ya jambazi huyo kuuawa, alipekuliwa na kukutwa na silaha hiyo Browning,
na pia alikutwa na sare za kampuni ya ulinzi zisizokuwa na nembo na
zenye rangi ya buluu bahari, fulana moja idhaniwayo ya Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na boti za kijeshi jozi moja, kamba ya
mkonge, plasta, bisibisi na maski za mdomo.
Aidha,
alisema sare za ulinzi alizokutwa nazo jambazi huyo ndizo zilizoonekana
kuvaliwa siku ya tukio la Kinondoni, huku mtuhumiwa aliyekamatwa awali
akikutwa na vibao vya namba za magari zenye namba za usajili STK 4704 na
T. 503 APG, vocha za Vodacom za Sh 5,000 pisi 10, tabuleti aina
Samsung, pasipoti mbili zenye majina ya Salum Malulu na Jeremiah Malulu
zenye picha ya mtu mmoja, kitambulisho kinachodhaniwa ni cha Usalama wa
Taifa na mihuri minne.
Alieleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwapata washiriki wote wa tukio hilo la mauaji ili wachukuliwe hatua za kisheria.