Jaji Mutungi Atishia Kuchukua Hatua Kali za Kisheria Dhidi ya CHADEMA na CUF
Siku
chache baada ya vyama vya upinzani vya Chadema na CUF (Upande wa
Profesa Ibrahim Lipumba) kutishiana kuharibiana kupitia oparesheni zao
mpya, msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amevionya
vyama hivyo.
Chadema
walikuwa wa kwanza kutangaza kuingilia mgogoro ndani ya CUF wakitangaza
kuanzisha ‘Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni’ wakilenga kumuondoa
mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili, Profesa Ibrahim
Lipumba.
CUF
inayomuunga mkono Profesa Lipumba pia ilijibu mapigo kwa kudai kuwa
itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’, wakilaani kitendo cha Chadema
kuingilia mgogoro huo.
Kufuatia
kauli hizo, Jaji Mutungi amevionya vyama hivyo kuwa vitakabiliwa na
mkono wa sheria endapo vitajihusisha na vurugu ya aina yoyote.
Msajili
aliongeza kuwa ingawa amesikia kupitia vyombo vya habari vitisho hivyo,
hajapokea barua yoyote ya malalamiko ofisini kwake kutoka kwa vyama
hivyo.
“Natoa
onyo kwa chama chochote cha siasa ambacho kitaonesha ubabe na kutumia
wafuasi wake waweze kufanya vurugu. Tutakichukulia hatua kali kwa mujibu
wa sheria,” Jaji Mutungi anakaririwa na Mtanzania.
“Kama
kungekuwa na tatizo wangeleta barua ofisini kwangu ya malalamiko,
lakini mpaka sasa sijapata barua yoyote inayohusiana na madai yao zaidi
ya kusoma kwenye vyombo vya habari,” aliongeza.
Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea alifanya mkutano na vyombo vya habari hivi
karibuni jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa wamebaini Profesa Lipumba
anatumika kuidhoofisha CUF hali itakayodhoofisha pia muungano wa Ukawa,
hivyo wameamua kumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif
Sharif Hamad.
Kubenea
alitangaza rasmi ‘Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni’ akidai kuwa tayari
ilishaanza wakiwa Bungeni mjini Dodoma kwa kuwatenga wote
wanaoshirikiana na Profesa Lipumba.
Saa
chache baadae, Naibu Katibu Mkuu CUF upande wa Bara, Magdalena Sakaya
ambaye anatambuliwa na Ofisi ya Msajili na anayemuunga mkono Profesa
Lipumba alijibu mapigo kwa kueleza kuwa kambi yake itakuja na
‘Oparesheni Futa Chadema’.