Ofisi ya CCM Yachomwa Moto Pwani
Watu
wasiojulikana wameichoma moto ofisi ya Chama cha Mapinduzi tawi la
Mshonzini iliyopo wilayani Mafia mkoani Pwani na kuteketeza mali
mbalimbali za chama hicho.
Akithibitisha
tukio hilo, Katibu wa CCM wilayani Mafia Mohammed Dhikiri amesema tukio
hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Alhamisi Julai 13.
Dhikiri amesema moto huo umeteketeza kabisa ofisi hiyo pamoja na samani za ndani.
Amesema
bado haijajulikana sababu za ofisi hiyo kuchomwa moto kwa kuwa wakati
tukio linatokea hakukuwepo na viashiria vyovyote vya vurugu miongoni mwa
wanachama.
Amesema
bado halijafahamika ni nani aliyehusika na tukio hilo na kueleza kuwa
wameliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi zaidi dhidi ya tukio
hilo.
Naye
Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau amesema vipo viashiria vinavyoonyesha kuwa
alifika mtu asiyejulikana karibu na ofisi hiyo kisha kuwasha na kurusha
kijinga cha moto kwenye paa la makuti la ofisi hiyo.
Dau
amesema mtu huyo baada ya kutekeleza kitendo hicho aliondoka kuelekea
kichakani kama ambavyo alama za nyayo za miguu yake zilivyoonyesha.
Amesema
hilo ni tukio la kwanza kutokea wilayani humo kwa kuwa hadi linatokea
hapakuwa na viashiria vyovyote vile vya kutokuwepo kwa Amani kati ya
wanachama au viongozi.