MWALIMU WA SEKONDARI MBARONI KWA KUMPA UJAUZITO MWANAFUNZI WAKE
POLISI mkoani Rukwa inamshikilia mwalimu wa Shule ya Sekondari Miangalua
iliyopo katika wilaya ya Sumbawanga akituhumiwa kumpatia ujauzito
mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 16, ambaye alikuwa akisoma kidato
cha tatu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kuwapo kwa
tukio hilo, akisema tayari mtuhumiwa huyo amekamatwa na anashikiliwa kwa
mahojiano na katika Kituo cha Polisi kilichopo katika mji mdogo wa
Laela wilayani Sumbawanga.
Atafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awali kukamilika
ambapo anatuhumiwa kwa makosa matatu ya kumpatia ujauzito mwanafunzi
huo, kumbaka na kukatisha masomo yake.
Akizungumzia mkasa huo, Mkuu wa shule hiyo, Gishi Milundi amekiri
kutokea kwa mkasa huo ambapo mwalimu wake anahusishwa na tuhuma hizo
huku akiongeza kuwa, baada ya kuhisiwa kuwa ana dalili za ujauzito
alikwenda kupimwa katika zahanati ya Miangalua na kubainika kuwa na
ujauzito wa miezi mitano.
IMEANDIKWA NA PETY SIYAME, SUMBAWANGA