Diwani Arusha aitosa Chadema akieleza anamuunga mkono Rais Magufuli
Diwani
wa Ngabobo (Chadema), Solomon Laizer ameandika barua ya kujiuzulu
udiwani na kujiunga na CCM kwa maelezo anamuunga mkono Rais John
Magufuli.
Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu kwa kutoa sababu kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli.
Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri amethibitisha jana
(Julai 11) kupata taarifa za kujiuzulu kwa Ngabobo.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema kujiuzulu kwa diwani huyo ni mchezo mchafu akidai amenunuliwa.
Amesema
tayari walipata taarifa za diwani huyo kushawishiwa kujiuzulu na
kwamba, alifuatwa na viongozi wa wilaya na kanda wa chama hicho
aliowaeleza kuwa ameshawishiwa.
"Baadaye
alieleza hataondoka lakini naona wamefanikiwa kumshawishi, tunashangaa
viongozi wa Serikali badala ya kufanya kazi za maendeleo wanafanya kazi
za kushawishi madiwani wa upinzani kuhama," amesema.
Hata hivyo, madiwani wanaohama wanapinga kuwa wameshawishiwa kufanya hivyo.
Hadi sasa madiwani watano wa Chadema waliojiuzulu ni Credo Kifukwe wa Kata ya Murieti jijini Arusha.
Wengine
waliojiuzulu katika Jimbo la Arumeru Mashariki na kata zao kwenye
mabano ni Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson
Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).