TRA yavuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka 2016/17
Mamlaka ya Mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni 14.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Makusanyo
haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.67 ikilinganishwa na makusanyo ya
mwaka 2015/16 ambayo yalikuwa ni kiasi cha Shilingi Trilioni 13.3.
Sambamba
na Makusanyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA Bw.
Richard Kayombo alisema Mamlaka imeendelea kukusanya kodi mbalimbali
ikiwemo kodi ya majengo na muitikio wake umekuwa ni wa kiwango cha
kuridhisha.
Mamlaka
inapenda kuwashukuru walipakodi wote kwa muitikio huo na wengine
wanaoendelea kujitokeza katika ofisi mbalimbali za Mamlaka nchi nzima
ili kuweza kulipa kodi hiyo ambayo mwisho wa kulipa kodi hiyo ni tarehe
15 Julai, 2017.
Aidha,
Mamlaka inapenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wote kutoa risiti za
EFD pindi wanapouza bidhaa au huduma na Wananchi wote kuhakikisha
wanadai risiti pindi wanaponunua bidhaa au kupata huduma na kuwa,
kinyume na hapo watakuwa wanatenda kosa kwa mujibu wa sheria ya
usimamizi wa kodi.
Hivi
sasa kuna zoezi la uhamasishaji na ukaguzi linaloendelea nchi nzima
katika sehemu zote za biashara kukagua wafanyabiashara wasiotumia
Mashine za Risiti za Kielektroniki za EFDs pamoja na wananchi wote
wasiodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma.
“Napenda
kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao ili kuona usahihi wa
tarehe na kiasi walicholipa kabla ya kuondoka na risiti hiyo” alisistiza
Kayombo
‘Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI