DC URAMBO ALILIA NA ZAO PAMBA
Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina
Kwinga, akizungumza na maofisa Ugani wa wilaya hiyo wakati akifungua
mafunzo ya siku moja kwa maofisa ugani kutoka kata zote na vijiji vya
wilaya hiyo wilayani humo leo.
Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo, Margareth Nakainga, akizungumza katika mafunzo hayo.
Picha ya pamoja kati ya Viongozi wa Wilaya ya Urambo,Watafiti pamoja na Maafisa ugani wa Wilaya hiyo.
*****
Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina
Kwingwa amewaomba watafiti wa kilimo toka Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia(COSTECH) pamoja na Kituo cha Utafiti Ukiriguru wawape elimu
nzuri ya kutosha katika kilimo cha zao la Pamba Maafisa Ugani wa wilaya
yake ili waweze kulima kilimo hicho na kiwe chenye tija kwao.
Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo wakati akifungua kifungua mafunzo ya siku moja kwa maofisa ugani kutoka kata zote na vijiji vya wilaya hiyo wilayani humo leo, yaliyolenga kukumbushana namna ya kulima kilimo cha kisasa na chenye tija kwa jamii ya sasa.
Angelina alisema pamoja na kwamba wilaya
yake inalima zao kubwa la tumbaku lakini bado wanahitaji kuwa na zao la
pamba pia lina manufaa kwao.
“Tunaomba watafiti mtusaidie kufundisha
hawa maafisa ugani kulima zao hilo la pamba,japo wao wanalima lakini
bado hatujafanya vizuri hivyo tunahitaji maafisa hao wapate mafunzo
katika zao hili ili tuanze kulima na tufanikiwe kama wilaya
nyingine”,alisema Angelina.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliwaomba
maafisa ugani kufanyia kazi mafunzo waliyopewa katika sehemu zao husika
ili yaweze kuzaa matunda kwao na kuboresha mazao ambayo wanalima sasa.
"Lakini pia niwaombe maafisa ugani
kuchukua fursa hii na kuelewa unakwenda kupambana vipi katika kituo
chako cha kazi ili kuanza kuleta mafaniko katika wilaya yetu na kuanza
kuwa na kilimo cha kisasa,na kama tusipoona matokeo tutajua nyinyi ndiyo
mtakuwa na matatizo na siyo wakulima",aliongezea Angelina.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
halmashauri ya Urambo Magreth Nakaingwa alibainisha kuwa ulimaji wa zao
moja kama vile wao wanavyotegemea Tumbaku kumesababisha wakulima wengi
kukosa namna ya kujikimu kimaisha kutokana na soko la tumbaku kushuka
kwa kasi.
“Uchumi wa wilaya ya Urambo unategemea
zaidi zao la tumbaku na msimu huu wa mavuno changamoto ambayo wakulima
wamekutanayo ni kwamba masoko yameenda polepole kwanza yamechelewa
kuanza lakini hadi sasa wakulima wa tumbaku hawajauza tumbaku katika
maghala yao”alisema Magreth.
“Kutokana na hali hiyo wakulima wengi
wamekosa fedha ambapo imewaathiri sana na sasa wanataka wakulima hao
kujikita katika mazao mengine ya biashara ili waweze kuwa na njia
nyingine ya kujipatia kipato”,alisema Magreth.
Hata hivyo Tume ya Taifa ya Sayansi
(costech ) kupitia Jukwaa la baiteknolojia nchini (OFAB)imesema
itaendelea kutoa mafunzo kwa maafisa ugani katika wilaya na mikoa
mbalimbali lengo likiwa ni kufanya kilimo kiwe cha kisasa ili kufikia
azma ya serikali ya awamu ya Tano ifikapo 2025 kuwa Tanzania ya viwanda.
Na Hellen Isdory - Urambo.