BODI YA MIKOPO YAWABANA WENYE VYETI FEKI....KAMA WALIKOPA LAZIMA WALIPE TU
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESB) imesema haijalishi
mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu alipatwa na kadhia ya vyeti feki au
alifeli shule na kusitishiwa masomo, ilimradi alikopa anatakiwa kulipa
deni lake.
Aidha, imeeleza kuwa hadi sasa imekwishakusanya Sh 216,992,990,52.98
kati ya Sh 427,708,285,046.48 za mikopo iliyoiva ambayo ipo tayari
kukusanywa. Pia imesema licha ya kuendelea kuwatafuta wadaiwa sugu
100,000 kwa sasa, marejesho iliyoyakusanya yameivusha kutoka kwenye
lengo ililojiwekea katika mwaka wa fedha 2016/17 la kukusanya asilimia
40 ya mikopo yote iliyoiva.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESB, Abdurazack
Badru alisema mafanikio hayo yametokana na hatua tatu kuu walizozichukua
kuhakikisha marejesho ya mikopo yanafanyika, ambazo ni pamoja na
kuwatafuta wadaiwa sugu wa kuanzia mwaka fedha 1994/95.
Alitaja hatua nyingine mbali na kutoa ankara kwa wadaiwa kuwa ni
kuwatafuta wanufaika, kupata taarifa zao muhimu pamoja na ukaguzi mahali
pa kazi. Kwa mujibu wa Badru, hadi kufikia Juni mwaka huu, wanufaika
139,259 walitambuliwa na kuanza kulipa marejesho ya mikopo yao.
Aliweka wazi kuwa waajiri hasa katika ofisi za umma ndio waliochangia
zaidi kupatikana kwa marejesho hayo kwa sababu ya wingi wa watumishi
waliokopeshwa ambao kwa namna moja au nyingine ‘wamewabana’ kuhakikisha
wanalipa mikopo yao.
“Sekta binafsi nayo imetusaidia ingawa kundi la waliojiajiri mfano
kuendesha bodaboda na wanaoendesha kilimo na ujasiriamali mwingine lenye
wanufaika 28,893 nalo limerejesha jumla ya Sh bilioni 13.7 na
kutuonesha mwitikio mkubwa zaidi,” alieleza.
Aliongeza kuwa bodi hiyo inapitia changamoto nyingi kukusanya marejesho
ya mikopo iliyoitoa kwa sababu baadhi ya waajiri hawana taarifa zao
zilizokamilika na sahihi huku wengine wakikata marejesho hayo kutoka
kwenye mishahara na kutoyawasilisha kwenye bodi hiyo kwa wakati au
kutoipeleka kabisa.
Alisema tayari imekwisha wafikisha mahakamani waajiri watatu ambao ni
kampuni kwa makosa hayo ya kukaa na fedha za marejesho ya mikopo ilhali
wamekwishayatoa kwenye mishahara ya wanufaika ambao ni waajiriwa wao.
Kwa maelezo yake, hadi sasa wanawatafuta wadaiwa sugu 100,000.
IMEANDIKWA NA NAMSEMBAELI MDUMA-habarileo
IMEANDIKWA NA NAMSEMBAELI MDUMA-habarileo