JINSI WENYE VYETI FEKI WANAVYOSHUGHULIKIWA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki
amesema watumishi wa umma walioghushi vyeti watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Kairuki amesema hayo jana (Julai 11)
katika kikao kazi na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Temeke, Tarafa ya Mbagala.
Alisema wote walioghushi vyeti hawapo kazini na wameshafutwa katika orodha ya malipo ya Serikali.
Waziri alielekeza waajiri kuwafuta wote
wasiostahili kuwepo katika orodha ya malipo na wasimsubiri hadi afike
katika maeneo yao ya kazi ili kutekeleza agizo hilo.
“Baada ya uhakiki kukamilika, hatua za
kinidhamu zitachukuliwa kwa walioghushi vyeti kwa kuzingatia sheria,
kanuni, utaratibu na miongozo iliyopo katika utumishi wa umma,” alisema
Kairuki kama alivyokaririwa katika taarifa iliyotolewa na wizara.
Aliwataka waajiri kuhakikisha wanahakiki
taarifa za watumishi wapya wanapoajiriwa na wale wanaohamia ili
kujiridhisha kama wana vyeti safi.
“Ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha
kuwa vyeti vya kila mwajiriwa mpya vinathibitishwa na mamlaka husika
kabla ya kumwajiri na hatimaye kumuingiza kwenye orodha za malipo ya
mshahara kupitia mfumo wa HCMIS na mifumo mingine ya mishahara ya
kitaasisi,” alisema.
Akizungumzia watumishi wa umma
walioajiriwa na sifa za darasa la saba, Kairuki alisema endapo
aliajiriwa kabla ya Mei 20 mwaka 2004 anastahili kuendelea kuwa katika
utumishi wa umma na endapo kajiendeleza abadilishiwe muundo kuendana na
sifa za elimu aliyopata.
Alisema endapo mtumishi huyo aliajiriwa baada ya Mei 20 mwaka 2004 anatakiwa kuwa na sifa ya elimu ya kidato cha nne.
Kairuki pia alitoa ufafanuzi wa kazi
inayoendelea inayohusu kuoanisha taarifa za watumishi na zile za usajili
uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
“Uhakiki huu utaongeza usahihi wa
taarifa za watumishi nchini, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa
taarifa zinazomhusu mtumishi na kutekeleza azma ya Serikali ya
kuunganisha mifumo ya kimkakati ya Tehama ili ibadilishane taarifa,”
alisema.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar e Salaam, Theresia Mbando alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuboresha utumishi wa umma.
Mbando alisema sasa watumishi wa umma
waliobaki kazini wameweza kuziba pengo la waliobainika kuwa na vyeti vya
kughushi na kuondolewa kazini.