Bodi ya mikopo yajipanga kutangaza vigezo vya wanufaika
Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema hivi karibuni
itatangaza sifa na vigezo vitakavyotumika kuwapangia wanafunzi mikopo ya
elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 unaotarajia kuanza miezi
michache ijayo.
Ufafanuzi
huo umetolewa jaa (Ijumaa, Julai 7, 2017) jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Dk Cosmas
Mwaisobwa wakati akijibu maswali ya baadhi ya wateja waliotembelea Banda
la HESLB katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako HESLB inashiriki
katika Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara.
“Tunakamilisha
mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka ujao wa masomo na tumepanga kabla
ya mwisho wa mwezi huu wa Julai tuwe tumeutangaza na tumefungua mtandao
wetu ili waombaji wenye sifa waombe,” alisema Dk Mwaisobwa.
Dk
Mwaisobwa amewataka waombaji wa mikopo watarajiwa wawe watulivu na
kufuatilia kwa karibu vyombo vya habari na tovuti ya HESLB
(www.heslb.go.tz) ambayo huwa na kiunganishi (link) cha mfumo wa kuombea
mkopo.
Awali,
katika maonesho hayo, baadhi ya wananchi wanaotarajia kuomba mikopo ya
elimu ya juu wamepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali yakiwemo
tarehe ambayo Bodi itaanza kupokea maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo
2017/2018.
Maswali
mengine yaliyoulizwa ni kama utaratibu wa udahili kupitia vyuoni moja
kwa moja utaathiri upatikanaji mikopo, wengine walitaka kupata elimu
zaidi kuhusu taratibu za urejeshaji wa mikopo.
Akifafanua
kuhusu maswali hayo, Dkt. Mwaisobwa alisema Sheria iliyoanzisha HESLB,
pamoja na mambo mengine, inamtaka mnufaika kuanza kurejesha mkopo wake
miezi 24 baada ya kuhitimu masomo.
Mkurugenzi
huyo wa HESLB alisema kuwa sheria hiyo inamtaka mwajiri yeyote
kuwasilisha kwa HESLB majina ya waajiriwa wake wote ambao ni wahitimu wa
taasisi za elimu ya juu ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri na Bodi
itamjulisha kama ni wanufaika au hapana pamoja na utaratibu na kiwango
cha kumkata mnufaika.
Dk
Mwaisobwa aliwataka wananchi kutembelea banda la HESLB kwa kuwa Bodi ya
Mikopo itaendelea kuonyesha shughuli zake kwenye banda lake lililopo
ndani, Banda la Benjamin Mkapa (Namba 19&20) hadi mwisho wa
maonyesho hayo, tarehe 13 Julai, 2017.