YANGA INA DAKIKA 360, IKIZITUMIA VIZURI BINGWA, LAKINI OMOG ANA HAYA YA KUSEMA
Bosi
wa benchi la ufundi la Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, ameweka
bayana kwamba hatishwi na idadi kubwa ya mechi zilizobakia kwa upande wa
wapinzani wao Yanga na badala yake yeye anaangalia kikosi chake jinsi
kitakavyoendelea kupata ushindi kwenye mechi zao.
Omog
jana alikiongoza kikosi chake kupata ushindi dhidi ya African Lyon na
kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kikiwa kimebakiza mechi
mbili.
Yanga mpaka sasa wamebakisha mechi nne zenye dakika 360 ambazo ni mbili mbele ya Simba.
Kocha
huyo amesema kuwa kwake wala hana neno na hali hiyo kwani anaamini Yanga
wanaweza kupoteza pointi kwa kuwa mechi hizo walizobakiza, baadhi ni
dhidi ya timu ambazo zinapigana kutoshuka daraja, hivyo hazitataka
kufungwa kirahisi.
Yanga imebakiza mechi dhidi ya Kagera Sugar, Mbeya City, Toto na Mbao.
“Kuwa
mbele ya Yanga kimichezo kwangu wala hakuna kitu kinachoniathiri kwa
sababu nimekita mawazo yangu katika kushinda mechi zetu na siyo
kumuangalia mpinzani wetu anafanya nini au kabakisha idadi ya mechi
ngapi.
“Kuwa
na mechi nyingi kwa sasa sidhani kama ndiyo watatwaa ubingwa kwa sababu
timu nyingi zinapigania kutoshuka daraja sasa unapokutana nazo zinacheza
kufa na kupona kuhakikisha kwamba huzifungi na jambo hilo ndilo
linalonipa imani kuwa wapinzani wetu hawatatufikia,” alisema Omog.