THAMANI
ya Ligi Kuu ya Kenya maarufu kama Kenya Premier League imekuwa ikipanda
kwa kasi kubwa na kuanza kurejesha heshima ya soka la Kenya.
Kabla,
soka la Kenya lilionekana limepoteza mvuto kabisa na kwa zaidi ya
misimu nane limekuwa likisuasua na kuandamwa na migogoro ya kila aina.
Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), chini ya mkongwe Sam Nyamweya lilionekana kupoteza mwelekeo na mambo yakazidi kuwa magumu.
Ilifikia wakati kukawa na ligi mbili ndani ya nchi moja. Ligi moja ilisimamiwa na FKF na nyingine bodi ya ligi.
Mwisho
wa msimu, kukawa na bingwa wawili, washindi wa pili wawili
halikadhalika watatu na wengineo. Hii ilikuwa ni sehemu ya kuonyesha
kwamba soka la Kenya limekosa mwelekeo kabisa.
Miaka
minne iliyopita wakati Nyamweya anakaribia kuondoka, timu ya taifa ya
Kenya “Harambee Stars” chini ya Kocha Adel Amrouche, ilifanikiwa kutwaa
ubingwa wa Kombe la Chalenji lililofanyika nchini humo.
Wengi
walishangazwa na sifa nyingi zikaenda kwa kocha Amrouche raia wa
Ubelgiji mwenye asili ya Algeria. Kwamba ana uwezo wa kufanya katika
mazingira magumu kama alivyokuwa akiifundisha Burundi.
Uchaguzi
uliofuata, Nyamweya aliangushwa na Nick Mwendwa, akiwa ni rais kijana
kushika nafasi hiyo. Wengi waliingiwa hofu angeweza vipi kuendesha mambo
naye alikubaliana na hali haikuwa nzuri.
Mwaka wa kwanza, hali ilionekana kuzidi kuwa ngumu na ule usemi kwamba angekwama ukazidi kuchukua nafasi.
Lakini wakati ikionekana na Mwendwa alikuwa ameshindwa, ghafla mambo yalibadilika na kuanza kwenda kwa kasi kubwa.
Wengi
wakaonekana kushangazwa kwa kuwa Kenya ilikuwa kati ya timu zilizokuwa
chini ya kiwango cha 130 katika viwango vya soka vya Fifa. Hawakuwa tena
na tofauti na Tanzania ambao angalau walikuwa na nafuu.
Utaona
ule mlolongo wa wachezaji wengi wa Kenya na hata Uganda kukimbilia
Tanzania ulizidi kuongezeka kwa kuwa hata zile timu kama Sofapaka
zilizokuwa zikilipa vizuri zilidorora na wakongwe Gor Mahia na AFC
Leopards walikuwa wameyumba na kuonekana hawana nafasi kwani kila
walipoinuka walianza kuyumba tena.
Mwendwa
akaonekana ni shujaa, lakini ukweli ni udhamini mnono ambao walianza
kuufanya kampuni ya masuala ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.
SportPesa
walidhamini timu zote kongwe mbili za Gor Mahia na AFC Leopard na
kawaida wao ndiyo chachu ya ushindani. Pia wakadhamini timu nyingine na
Nakuru All Stars.
Kama
hiyo haitoshi, kampuni hiyo ikaingiza udhamini mnono katika Ligi Kuu
Kenya na kufanya kuwe na ushindani zaidi kwa kuwa fedha hizo zinaingia
kwenye mifuko ya timu zote 18 zinazoshiriki ligi hiyo.
Ukiangalia
thamani ya ligi ya Kenya imepanda, ushindani umerudi na hamasa hata ya
mashabiki kwenda viwanjani imerudi kwa kasi kubwa na sasa ni kati ya
ligi zilizo juu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Taarifa
zimekuwa zikieleza SportPesa tayari wako nchini na wamenuia kuzidhamini
Yanga na Simba ambazo ni timu zenye mashabiki zaidi katika ukanda huu.
Inawezekana siku moja wakaingia kwenye ligi lakini kampuni hiyo kama itatumika vizuri basi inaweza kurejesha hamasa tena.
Huenda tuaona kawaida lakini mfano mzuri, Simba kwa msimu mzima wa 2016-17 imecheza kwa hasara kama tulivyowahi kuandika makala.
Kwamba
hawana mdhamini na vifua vyao ni mali, lakini hakukuwa na aliyeona
thamani yao baada ya kujiondoa kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Shukrani
kwa TBL kwa kuwa waliweza kujali angalau kwa misimu kadhaa. Lakini kama
SportPesa basi ndiyo wakati mwingine wa kurejesha heshima ya soka
nchini.
Hakuna unapoweza kukwepa fedha katika maendeleo ya soka. Vizuri pia kufanya kazi na watu waliojifunza kupitia hatua mbalimbali.
Mfano
SportPesa wanadhamini timu ya Ligi Kuu England (EPL), Hull City.
Unapozungumzia udhamini wanajua nini cha kufanya kusaidia zaidi.
Kawaida
wadhamini walioendelea hupenda mafanikio kwa wale wanaowadhamini. Hii
ni nafasi kwa Yanga na Simba kubadili mambo na hasa kama wataingia
udhamini, basi fedha watakazozipata ziwe kwa ajili ya maendeleo na si
mifuko ya wahusika.
SportPesa
ni sehemu wa wadhamini wa klabu maarufu ya Arsenal ya England. Hivyo
wanajua kitu kinachoweza kuwasaidia Yanga na Simba lakini soka la
Tanzania.
Kikubwa
ambacho SportPesa wamekuwa wakikifanya ni kurudisha kiasi cha fedha kwa
jamii kama udhamini. Wameweza kuzirudisha Gor Mahia na AFC Leopards
katika ramani ya soka zikiwa na nguvu.
Simba
na Yanga hazikuwa zimekufa lakini mwendo wao ulikuwa unaashiria “kifo”.
Sasa ndiyo wakati mwafaka wa kutumia vizuri udhamini huo unaelezwa kuwa
utakuwa mkubwa zaidi kuliko waliowahi kupata hapo awali.
SOURCE: CHAMPIONI