Mbunge wa Korogwe Vijijini akisaidia wananchi
wake kutokana na mafuriko yaliyolikumba jimbo hilo kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha.
IDADI ya wakazi waliokufa kutokana na athari za mvua ya masika
inayoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali wilayani Korogwe Mkoa wa
Tanga, imefikia saba sasa wakiwemo wanawake watano, wanaume wawili
pamoja na majeruhi 10, huku barabara ya Segera – Mkumbara ikifungwa kwa
muda.
Vifo hivyo vyote vimetokana na maporomoko ya maji, mawe, miti na mchanga
kutoka katika Milima ya Usambara Magharibi ambavyo vimeendelea kuvamia
kwa kasi baadhi ya nyumba zilizo mabondeni katika kata za Mkumbara,
Chekereni, Makuyuni, Kwagunda, Kerenge na Ngombezi.
Pia Imebainika kwamba hali ya usalama kwa baadhi ya wananchi imekuwa
tete hasa wale wanaokaidi agizo la serikali linalowataka kuhama badala
yake wanaendelea kung’ang’ania kuishi ndani ya nyumba zao zilizoko
bondeni jirani na kingo za Mto Pangani kwa kuwa tayari wanyama wakali
akiwemo mamba wameanza kutumia mafuriko hayo kuvamia nyumba hizo ili
kutafuta malisho.
Akizungumza jana jioni katika mahojiano kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya
ya Korogwe, Robert Gabriel alisema hali ya uslama kwa wakazi wa maeneo
hayo haijatengemaa hivyo jamii inapaswa kufanya kila linalowezekana ili
kuokoa maisha.
“Kuna tukio la kusikitisha sana la jana huko Kata ya Ngombezi ambako ni
jirani na mto Pangani kuna mama mmoja amenusurika kuliwa na Mamba wakati
alipokuwa akisafisha kifaa cha kudekia nyumba kwa kutumia maji hayo ya
mafuriko,” alisema mkuu wa wilaya na kuongeza: “Ilikuwa tu baada ya
kumaliza usafi akaamua kwenda kusuuza dekio bila kujua kwamba kumbe
mamba alikuwa mawindoni ametoka huko mtoni na kujichanganya kwenye hayo
mafuriko jirani na nyumba wakati mama akiendelea kusafisha ndipo mamba
akavamia hilo dekio na kuondoka nalo na mama akanusurika.
Hii ni hatari nawahimiza watii agizo la serikali ili tuokoe maisha kwa
kukubali kuhamia maeneo makavu ya juu milimani.” Alisema kitendo cha
mama kuvamiwa na mamba kutokana na mafuriko kuendelea kuzingira nyumba
ni kiashiria tosha kwamba maji yanapoingia ndani na mamba nao wanahamia
katika makazi ya wananchi hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuchukua
tahadhari.
Aidha, alitaja athari nyingine zilizopatikana ni kufungwa mara kwa mara
kwa baadhi ya barabara kuu na kusababisha baadhi ya magari na watumiaji
wengine kusubiri kwa muda wakati maporomoko ya maji na mawe yanapokatiza
kwenye maeneo hayo.
Alisema mpaka sasa tathmini halisi ya hasara iliyosababishwa na maafa
hayo bado haijapatikana kwa kuwa kamati ya wilaya inatarajia kukutana
kesho. Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani
Tanga, Alfred Ndumbaro akizungumzia madhara yaliyotokea katika baadhi ya
barabara kuu kutokana na mafuriko hayo, alisema wao wamefanikiwa
kuondoa vikwazo barabarani ili gari ziendelee kupitika.
“Kikosi kazi chetu kinashughulikia maeneo ya Mazinde na Mkumbara katika
barabara kuu ya Segera - Mkumbara ili kuhakikisha miundombinu hiyo
inarejea katika matumizi yake ya kawaida,” alieleza Ndumbaro baada ya
magari kukwama kwa muda eneo la Mazinde.
Hata hivyo, alitaja maeneo mengine ambayo yanaendelea kushughulikiwa ni
katika barabara kuu ya Mombo - Lushoto ambako vifusi vya udongo
vilianguka kutoka juu milimani na kuziba njia katika baadhi maeneo.
Kuhusu barabara kuu ya Tanga – Pangani, alisema Tanroads inafanya juhudi
za haraka za kuchepusha barabara katika maeneo yaliyoharibika ikiwemo
karibu na daraja la Neema ili kuwezesha watumiaji kuendelea kupata
huduma wakati serikali ikiangalia njia ya muda mrefu ya kutengeneza eneo
hilo.
Mmoja wa wasafiri waliokuwa wakitoka Moshi, Jacob Tesha alieleza kuwa
walikwama Mazinde tangu saa tano asubuhi, na walipewa taarifa na Polisi
wa Mazinde kuwa Mombo barabara imeharibika na magari yamezuiliwa na wao
walizuiliwa Mazinde. Alisema foleni ilikuwa ya mamia ya magari.
Alisema njia ilianza kufunguliwa saa 11 jioni, na akaeleza kuwa
makalavati ya eneo la Mombo ni madogo, hivyo maji yamefurika na kuharibu
njia. Wakati huo huo watu watano wamejeruhiwa na kulazwa katika
hospitali ya wilaya ya Lushoto baada ya magari matano waliyokuwa
wakisafiria kati ya miji ya Soni na Lushoto mkoani Tanga kuangukiwa na
kifusi cha udongo na mawe.
Magari hayo ambayo namba zake za usajili hazikuweza kupatikana mara moja
ni mabasi mawili aina ya Costa, Toyota Carina moja, Noah moja pamoja na
Hilux moja ambayo inamilikiwa na shirika La umeme Tanesco wilayani
Lushoto.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amethibitisha tukio
na kuongeza usiku huu jana askari wa jeshi la Polisi wilayani Korogwe
wamelazimika kufunga baadhi ya maeneo ya barabara kuu ikiwemo ya Mombo -
Mkumbara - Mazinde wilayani Korogwe ili kuepusha madhara kutokana na
ongezeko la maporomoko ya maji, tope, na miti kufuatia mvua nyingi
zinazoendelea kunyesha.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE- HABARILEO TANGA.