CCM ZANZIBAR YAWAFARIJI WAATHIRIWA WA MAFURIKO
Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma akipokea maelezo
kutoka kwa viongozi wa mtaa akiwemo sheha wa shehia ya Tomondo, Mohamed
Omar katika eneo la Ziwa maboga ambapo zaidi ya nyumba 200 zimeathiriwa
na mvua za masika zinazoendelea kunyesha.
Nyumba mbali mbali zilizoathiriwa na maji ya mvua katika eneo la Tomondo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Nyumba zilizovamiwa na maji katika eneo la Meli nne Makaburini Unguja.
Katibu wa Tawi la CCM Tomondo, Hassan Kipanga Abdalla akimweleza Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar hali ya waakazi wa shehia hiyo kutokana na
mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Abdalla Juma Saadala akiwafariji
wananchi wa eneo la Mwanakwerekwe Meli nne, waliopata maafa kutokana na
mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa.
Naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala akimfariji
mmoja wa wananchi ambaye nyumba yake imeporomoka kutokana na mvua za
masika zinazoendelea kunyesha hivi sasa nchini, uko Fuoni Migombani
Zanzibar.
……………………………………..
ZAIDI ya Nyumba 300 katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi
zimeathiriwa na Mvua za masika zinazoendelea kunyesha hivi sasa.
Akizungumza katika mtaa wa ziwa maboga sheha wa shehia ya Tomondo, Bw.
Mohamed Omar Said alisema zaidi ya nyumba 200 katika eneo hilo
zimeathiriwa na mvua kwa kujaa maji na zingine kuporomoka.
Bw. Said alifafanua kwamba baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wamehama
katika makaazi yao na kuomba hifadhi katika maeneo mengine yaliyokuwa
salama, huku idadi ya nyumba zinazoathiriwa na mvua hizo zikiendelea
kuongezeka kadri mvua zinavyioendelea kunyenyesha.
Mbali na maeneo hayo pia katika mitaa ya Meli nne, Fuoni janga mizini na
Fuoni Migombani kuna nyumba zaidi ya 100 zimeathiriwa na mvua hizo.
Akizungumza juu ya athari hizo, Mjumbe wa sheha wa shehia ya kibondeni,
Bi. Zuhura Ame alisema hali za baadhi ya wananchi waliopata maafa hayo
sio nzuri hivyo wanahitaji msaada wa dharura.
Alisema kwamba licha ya viongozi wa majimbo hasa Wabunge, wawakilishi na
madini baadhi yao tayari wameanza kutoa msaada na wengine ndio
wanajipanga kufika kwa ajiri ya kuwafariji wananchi lakini bado
panahitajika nguvu za pamoja baina ya wananchi, vyama vya kisiasa na
serikali ili kuinusuru nchi kuingia katika maafa makubwa.
Naye Mkaanzi wa Mwanakwerekwe, Mwajuma Salum aliomba serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara inayohusika na masuala ya Miundombinu
kutoa kipaumbele cha kujenga madaraja makubwa na yenye viwango katika
maeneo mbali mbali nchini ili kuepusha hasara inayotokana na mvua hizo
kila mwaka.
“ Tumesikia juzi tu serikali yetu imetangaza bajeti ya mwaka inayofikia
Trioni moja, hivyo tunaomba kama inawezekana baadhi ya fedha zitumike
katika uimarishaji wa miundombinu yetu kwani wengi tunateseka kwa sasa,
mfano pale Mwanakwerekwe Gari za Shamba kuja mjini ni tabu kwani pale
katika Bwawa la maji hakupitiki.”, alisema Mwajuma.
Alisema licha ya serikali kufanya ziara katika maeneo hayo bado baadhi
ya wananchi hawana makaazi ya kuishi hivyo wanaiomba serikali iwapatie
misaada ya dharura ili nao wapate huduma muhimu kwa kipindi hichi
kigumu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “
Mabodi” aliwaagiza viongozi wa Serikali za Mitaa Zanzibar kuacha tabia
ya kuruhusu uuzaji wa viwanja na ujenzi katika maeneo hatarishi hasa
mabondeni na sehemu zinazotwaama maji ili kuepuka athari za mafuriko
zinazoweza kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Maelekezo hayo aliyatoa katika Mtaa wa Tomondo Ziwa maboga na maeneo
mengine wakati katika ziara yake ya kuwafariji wananchi waliopata athari
za mafuriko katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Alisema wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kujilinda dhidi ya
maisha yao kwa kuchukua tahadhari ya kutoishi katika maeneo wanayojua
kuwa ni hatari juu ya afya na maisha yao.
Aliahidi kwamba CCM kwa kushirikiana na serikali inaendelea kutafuta
ufumbuzi wa kuwasaidia wananchi waliopata athari hizo kwa Unguja na
Pemba.
“ Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi natoa pole sana kwa wananchi wetu wa
Zanzibar kwa Unguja na Pemba walioathiriwa na mvua hizi zinazoendelea
kunyesha hivi sasa, kwa upande wa CCM tutaendelea kuwa nanyi kwa kutoa
msaada wa Ari na Mali ili kuhakikisha mnarudi katika hali yenu ya
kawaida.
Pia nakuombeni wananchi ifikie wakati na sisi tuisaidie serikali yetu
kwa kuepuka kuishi ama kununua sehemu ambazo tunajua kwamba hazifai
kuishi binadamu wakati mvua zinapoanza kunyesha.”, alisema Dkt. Mabodi
na kuongeza kwamba CCM itaendelea kuwa karibu zaidi na wananchi kwa
lengo la kuwapunguzia changamoto hizo.
Dkt. Mabodi aliishauri serikali kuchukua hatua za haraka za kurekebisha
miundo mbinu ya barabara, maji na umeme kwa baadhi ya maeneo yaliyokubwa
na mafuriko hayo ili wananchi waendelee kupata huduma muhimu za
kijamii.
Aidha alitoa wito kwa wananchi ambao kwa sasa makaazi yao bado yapo
salama kujitolea kwa kuwasaidia wenzao waliopata maafa huku Chama kwa
kushirikiana na serikali wakitafuta njia mbadala za kusaidia katika
maeneo hayo.
Sambamba na hayo aliitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutembelea
katika maeneo yaliyopata athari hizo kwa kugawa dawa za kutibu maji ya
kunywa sambamba na kutibu visima ambavyo maji yake hayo salama kwa lengo
la kuwanuru wananchi wasipate maradhi ya miripuka kwa kipindi hichi cha
kuelekea katika Mwezi wa Ramadhani.
Alisema sululisho la kumaliza tatizo la maafa hayo yanayotokea kila
mwaka ni lazima wananchi waache kujenga katika mitaro ya kusafirisha
maji, hali inayosababisha maji hayo kukosa njia za kupita na kuwaathiri
wananchi wengine wasiokuwa na hatia.
Naibu Katibu Mkuu huyo, Dkt. Mabodi katika ziara hiyo amefuatana na
uongozi wa Mkoa wa Magharibi na Wilaya ya Dimani akiongozwa na Mwenyeji
wake Mwenyekiti wa Mkoa huo , Yussuf Mohamed Yussuf na alitembelea
maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi mengi yakiwa katika Wilaya
ya Maghatibi ‘’B” ambayo ni Tomondo, Mwanakwerekwe Sokoni,
Mwanakwerekwe Meli nne, Fuoni Migombani na Fuoni Chunga.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.