Serikali
imeendelea kuchukua hatua kwa kuendelea kutoa elimu katika Halmashauri za
Wilaya, Manispaa na Miji 72 ili kuondokana na tatizo la ndoa za utotoni zinazobababisha
watoto kukosa haki ya msingi ya kupata elimu.
Akijibu
swali la Mhe. Anna Kilango Malecela Mbunge wa Viti Maalum (CCM)lililouliza Je,
Serikali ina Mkakati gani wa kutokomeza ndoa za utotoni? Naibu Waziri wa Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsi Wazee na Watoto amesema kuwa msisitizo utazidi kuwekwa
katika utoaji wa elimu kwa familia, wazee wa mila na jamii kwa ujumla.
“Tutajikita
kutoa elimu zaidi ili jamii iachane na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati
za kuoza watoto wa kike” alisisitiza Mhe. Dkt. Kigwangalla.
Ameongeza
kuwa Serikali inatambua athari kubwa zinazosababishwa na ndoa za utotoni katika
jamii ya watanzania na itaongeza nguvu katika kutoa elimu na kupambana na wale
wote watakaojihusisha kwa namna moja au nyingine kuwanyima watoto wa kike haki
yao ya kupata elimu.
Aidha
kulingana na takwimu za Afya na Idadi ya Watu nchini za mwaka 2016 ndoa za
utotoni zimeshamiri katika mikoa ya Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora kwa
asilimia 58, Mara kwa asilimia 55 na Dodoma kwa asilimia 51 hivyo Serikali
itaendelea kupambana kutokomeza ndoa za utotoni nchini.
Kwa
upande wa muundo wa kisera na kisheria, Serikali imezifanyia maboresho Sera na
Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni pamoja na
marekebisho ya Sheria ya Elimu Sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo
kisichopungua miaka 30 kwa mtu yoyote atakayempa mimba mwananfunzi wa shule ya
Msingi au Sekondari.
Katika
kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali itaanza utekelezaji wa Mpango Kazi
wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha Sekta
zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili
na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.