MAJAMBAZI WATATU WALIOVAA HIJABU WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI PWANI
Watu
watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na
polisi baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kusimama eneo la kizuizi cha
Mwembe Muhoro wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Watu hao walikuwa wamepakiana kwenye pikipiki moja huku wakiwa wamevaa hijabu.
Akizungumza
na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, kamanda wa Polisi
mkoani Pwani ,Onesmo Lyanga alisema pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa
kukimbia.
Akielezea
juu ya tukio hilo alifafanua,lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya
mchana ,Muhoro ,Rufiji barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.
“Siku
ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu
zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila
moja “
“Miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.
Alisema
askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na
kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo
waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi
kusimama.
“Baada
ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na
kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro “
“Hata
hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari
waliwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga
risasi hewani,” alisema Lyanga.
Aidha
alibainisha baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza
kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na
kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.
“Majeruhi
hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika
na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya
Boxer yenye rangi nyeusi”
“Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.
Lyanga alisema walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia .
Hata
hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili
zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili
wawakamate.
Aliwataka
wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya
kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika
kukabiliana na uhalifu.