KWA NINI YANGA IMLIPE CHIRWA? WACHEZAJI WALIKWENDA WAKIWA TAYARI KUFUNGWA!
Na Saleh Ally
YANGA
wamefungwa mabao 4-0 katika mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho (Caf)
na sasa Tanzania haina mwakilishi tena katika michuano ya Caf katika
ngazi ya klabu.
Kipigo hicho kinaifanya Yanga iwe imetoka kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya ushindi wa bao 1-0 jijini Dar es Salaam.
Katika
mechi ya jana, kwa yule aliyebahatika kuiangalia atakubaliana na mimi
kwamba Yanga walisafiri wakienda kufungwa Algeria, walijua na walikuwa
na uhakika.
Kwanza
waliondoka wakiwa tayari wameanza kutanguliza madai yao ya mishahara ya
mwezi mmoja mmoja. Wapo wachezaji waliobadili uamuzi wa mgomo baada ya
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kwenda kuzungumza na wachezaji katika
mazoezi ya mwisho na kuwaeleza kilichomtokea akisisitiza uvumilivu
lakini akawaahidi hakuna haki yao itakayopotea.
Lakini
bado uchezaji wa kikosi cha Yanga ulionyesha upungufu mwingi na
hakukuwa na morali. Timu ilicheza ikionyesha haina kiongozi na hakika
haikuwa imejiandaa kushinda.
Huenda
walitaka kujaribu kuangalia kama itawezekana kushinda. Lakini walijua
watafungwa, hawakuwa na furaha na hawakuwa tayari kuipigania Yanga kwa
asilimia mia.
Mchezaji
kama Obrey Chirwa yeye aliamua kung’ang’ania pasi yake ya kusafiria,
akikataa viongozi wa Yanga kuichukua kwa ajili ya maandalizi ya safari
hadi atakapolipwa mshahara wake anaodai.
Yanga
ilimhitaji kwa kuwa alikuwa ndiye mshambulizi mwenye kiwango cha juu
baada ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma kuumia. Mechi ya juzi wamecheza
wakionekana wazi hawakuwa na msaada hata kidogo.
Ngoma
na Tambwe si wale waliozoeleka, wanahitaji mechi moja mbili, tatu
kuanza kurudi vizuri. Chirwa angeisaidia Yanga, lakini akasahau hata
alipotua nchini hakuwa na msaada licha ya kusajiliwa kwa zaidi ya Sh
milioni 150.
Anajua
alikaa benchi, alishindwa kufunga mechi kadhaa. Yanga wakaendelea
kumvumilia lakini baada ya kuonekana tegemeo kashindwa kuonyesha
uvumilivu, jambo ambalo linashangaza na Yanga wanashindwa kuonyesha wao
ni klabu. Jiulize, alipwe wa nini sasa? Kwenye mshahara wa Aprili,
hakuwa kazini bila ruhusa ya mwajiri. Sasa kwa nini alipwe?
Bao la kwanza:
Wakati
Mohamed Derrardja anapiga krosi na mpira kuguswa na Said Juma ‘Makapu’,
unaona mmaliziaji Said Aouedj anatokea nyuma ya Mwinyi Haji, anamalizia
wavuni.
Mwangalie Mwinyi, anageuka kama kitu kisichomuhusu akijua wazi hakuwa amemkaba mtu ambaye amekimbia na kufunga mbele yake.
Bao la pili:
Safari hii Mohamed Derrardja ambaye ni mtaalamu wa kupiga mipira iliyokufa wa MC Alger,
anafunga kwa mkwaju wa adhabu. Unaweza kushangazwa na Yanga waliokubali
kumuweka Hassan Kessy kwenye ukuta. Lakini kuonyesha hakuna tahadhari
au mafunzo ya kutosha, Kessy aliruka na kuondoka kwenye ukuta. Mpigaji
akatumia nafasi hiyo kufunga kirahisi kabisa na kipa Deogratius Munishi
‘Dida’ hakuwa na nafasi ingawa ukiangalia bila kupima unaweza kuamini ni
uzembe wake.
Kessy
ni mfupi, angeweza kutolewa na kwenda mbele kama namba tisa wakati
Ngoma na wengine wote wakirudi nyuma. Baada ya Yanga kupata mpira
anashuka katika nafasi yake wanakwenda kushambulia. Ilikuwa lazima
kujilinda na mapigo ya faulo ya Waarabu hao kwa kuwa wanajulikana.
Bao la tatu:
Zacharia Mansour ndiye alifunga bao la tatu akipokea krosi ya Hadj Bougueche, Dar walimtunga jina la “Mwarabu Mweusi”.
Bougueche
alitokea nyuma ya Kessy wakati krosi inapigwa ambaye hakugeuka wala
kutaka kujua nini kinatokea nyuma yake. Lakini wakati Mansour anafunga
Yanga ilikuwa na wachezaji watatu ndani ya boksi, lakini hakuna
aliyekuwa na msaada na kipa.
Bao la nne:
Huenda
hili ndiyo bao lililodhihirisha Yanga walikuwa tayari kufungwa Algeria.
Wakati Aouedj anafunga, utaona hivi, kulikuwa na wachezaji nane wa
Yanga pamoja na kipa wakiwa wamewazunguka wachezaji watatu wa MC Alger.
Wanne
akiwemo Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Kessy na Makapu walikuwa
wanatembea kama vile mechi ilishakwisha! Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin
Yondani na Mwinyi walijaribu kupambana kuzuia, wakazidiwa ujanja.
Yanga walishafungwa tatu, kweli walikuwa wametolewa lakini walikuwa na jukumu la kuzuia mabao kuendelea kuingia.
Lwandamina:
Kocha
George Lwandamina anapiga makofi tu baada ya Yanga kufungwa bao la
pili, haumuoni kuchangamka na kuwaita wachezaji na kuanza kuwapa
maelekezo ya haraka na kipi walikosea.
Wakati
mwamuzi anasumbuka kuwarudisha wachezaji wa MC Alger uwanjani, wakati
huo ulikuwa ni wa Lwandamina kuanza kuzungumza na wachezaji kuhakikisha
hawarudii makosa yanayofanana si kuendelea kupiga makofi akiamini ndiyo
hamasa.
Kiongozi:
Kila bao lililofungwa, wachezaji wa Yanga walionekana “wamekufa” kabisa. Hakuna wa “kuwafufua”, kocha alikuwa anapiga makofi tu!
Lakini
nahodha je? Kuwaita wenzake angalau kuzungumza nao au kuwapigia kelele
kuendelea kujitahidi ikiwezekana kuwakumbusha kuhakikisha wanapambana
zaidi wasikumbane na aibu ya kufungwa mabao mengi? Yote hii haikuwa sawa
na imechangia wao kufungwa mabao mengi zaidi na utaona makosa
yanafanana kwa kuwa hakukuwa na kukumbushana kwa kutosha.
Inawezekana
kuna matatizo ya uongozi, ya wachezaji nayo yameonekana. Lakini tayari
Yanga imepoteza uvumilivu miongoni mwao, itakuwa aghalabu kuwa na umoja
na inaonekana wazi hakuna upendo.
Uongozi wa klabu hiyo ukishindwa kufungua macho mapema, basi adhabu, maumivu na mateso ya kila mara yataendelea sana tu!